Watu 50 wamefariki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya boti kuzama kwenye mto kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Richard Mboyo Iluka, naibu gavana wa jimbo la Tshuapa, boti hilo lilikuwa limewabeba abiria wengi, wengi wao wafanyabiashara, waliokuwa wanasafiri kutoka eneo la Monkoto kwenda Mbandaka.

Amesema watu wengine 50 wamenusurika.

Gavana huyu amesema hadi sasa hawajafahamu chanzo cha ajali hiyo.

Kwa sasa maafisa wakuu wa jimbo hilo wamesafiri kwenda eneo la ajali kufahamu zaidi kuhusu idadi rasmi ya waliofariki na watu ambao walikuwa ndani ya boti hilo.

Bw Iluka ameambia mwandishi wa BBC Mbelechi Msochi kwamba Idadi rasmi ya waliofariki bado haijajulikana na uchunguzi unaendelea.

Kufikia sasa, miili iliyokuwa imepatikana ni 49 na kuna wasiwasi kwamba huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.

Mamia ya watu hufariki kila mwaka nchini DRC katika ajali za boti

Sababu kubwa zaidi huwa ni kubeba abiria kupita kiasi pamoja na nyingi za boti kuwa bovu. Boti nyingi huwa pia hazina maboya ya kutumiwa na abiria kujiokoa ajali inapotokea.

Mji wa Mbandaka kwa sasa unakabiliana pia na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na kuna wasiwasi kwamba ugonjwa huo unaweza kuenea kutoka mji huo wenye wakazi takriban milioni moja kwenda mji mkuu Kinshasa kupitia Mto Congo.

Mwezi jana, watu wengine zaidi ya 40 walikufa maji wakisafiri kuelekea taifa jirani la Congo-Brazzaville.

Please follow and like us:
Pin Share