Watu watano wauawa kwa shambulio la risasi Maryland Marekani

Polisi katika jimbo la Maryland nchini Marekani wanasema watu watano wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la risasi lililofanyika katika ofisi za kampuni ya Capital Gazette inayomiliki magazeti ya kila siku katika mji wa Annapolis.

Wafanyakazi wa gazeti hilo wanasema mshambuliaji huyo ambaye ni mzungu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 ambaye alijiharibu vidole vyake ili kuepusha kutambulika kwa alama za vidole alifyatua risasi hovyo kupitia mlango wa vioo.

Tiyari amekamatwa na polisi.

William Krampf ambaye ni Msaidizi mkuu wa polisi wa Anne Arundel amesema kwamba wamekuta pia vitu vilivyokuwa na muonekano wa vilipuzi na kuvidhibiti kwa haraka.

Ameongeza kwamba watu zaidi ya 170 waliokuwa katika jengo hilo walisindikizwa na polisi katika kuhakikisha wanakuwa salama kutoka katika jengo hili ambalo pia lilikuwa na biashara nyingine.

Kupitia mtandao wa twiter wanahabari kadhaa waliokuwa katika ofisi hiyo akiwemo Jimmy DeButts ambaye ni mhariri mkuu katika kampuni ya Capital Gazette wameelezea masikitiko yao kufuatia vifo vya wenzao huku wengine wakisema kwamba walikuwa ni kama ndugu zao.

Mashirika ya upelelezi ikiwemo shirika la FBI pamoja na taasisi inayoshughulikia masuala ya vileo, tumbaku ,silaha pamoja na vilipuzi wanashiriki katika uchunguzi wa tukio hilo.

Idara ya polisi ya mjini New York baadaye ilisema kwamba imepeleka maafisa na wataalamu wanaodhibiti masuala ya ugaidi katika mashirika ya habari mjini New York katika kuhakikisha kuwepo kwa usalama katika maeneo hayo.

Katika mtandao wa twitter Gavana wa Jimbo la Maryland, Larry Hogan amelitaja tukio hilo kama tukio baya na linalosikitisha kabisa na kwamba anashirikiana kwa karibu na Mamlaka husika.

Rais Donald Trump aliarifiwa kutokea kwa shambulio hilo na katika mtandao wake wa twitter ameandika kuwa anaziombea familia zilizopoteza ndugu zao na pamoja na wote walipatwa na janga hilo.

2263 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Tags :
Show Buttons
Hide Buttons