url-6Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wanatuhumiwa kutumia nyadhifa zao kupora shamba la hekari 74.2 mali ya Mwenegowa Mwichumu mkazi wa Kibada Kigamboni Dar es salaam.

Kabla ya uporaji huo shamba hilo lililokuwa na miti ya minazi, michungwa pamoja na miti mingine ambayo imeharibiwa na watu hao waliojimilikisha eneo hilo bila ya kufuata taratibu za kisheria.

Akizungumza na JAMHURI nyumbani kwake Kibada Mwinchumu anasema wafanyakazi hao kwa kuongozwa na ofisi ya kamishna wa ardhi kanda ya Dar es salaam kwa makusudi wameamua kupora eneo lake kwa kutumia vyeo vyao bila ya kufuata kama sheria inavyotaka.

Mwinjuma anasema katika tathmini hiyo mazao yake yalipewa bei ndogo tofauti na hali halisi na kupelekea eneo kufunguliwa jarada lenye kumbukumbu VAL/ PD/KB/1755 /Mgogoro namba 284 unatokana na mradi wa upimaji wa viwanja 20,000 katika Kata ya Kibada iliyopo katika Wilaya ya Kigamboni.

Anasema hayo yalitendeka mwaka 2004. Katika zoezi hilo maeneo mbalimbali yalifanyiwa tathmini na fidia kulipwa kwa kufuata taratibu za kisheria bila ya ubaguzi tofauti na hali ilivyokuja kutokea kwake.

“Cha ajabu walipofika katika eneo langu tathmini na upimaji ulifanyika kwa kiwango cha chini kwa kupunjwa eneo kubwa bila ya kuyafanyia tatmini hata mazao yaliyokuwemo ndani ya shamba hali ambayo sikukubaliana nayo,” anasema Mwinchumu.

Anasema pamoja na eneo lake kuwa na ukubwa hekari 74.2 lakini maofisa hao toka Wizara ya ardhi walibadili makadirio ya hekari 34 tu bila ya kutoa sababu za kuacha kupima eneo lote.

“Hapo ndipo mgogoro ulipoanzia nilipogoma kukubaliana upimaji wao ndipo wakaongeza hekari 10 kutoka za awali na kuwa 44 nilipo hoji sababu za kuacha kupima eneo lingine sikupewa majibu” anasema Mwinchumu.

Mwinchumu anasema maofisa hao mara baada ya kuona kwamba njama zao tayari amezishitukia wakalazimika kuahirisha zoezi na kupanga kuendelea siku nyingine.

“Baada ya mvutano wa muda mrefu na maofisa hao kwa mara nyingine upimaji ukapangwa kufanyika tarehe 21/3/2011 na mara hii upimaji wao ukaonyesha kuwa eneo hilo lina ukubwa wa hekari 74.2,” anasema Mwinchumu.

Anaeleza kwamba mara baada ya upimaji huo maofisa hao toka Wizarani walimuita ofisini na kuanza kumshawishi akubali kupokea hundi ya shilingi milion 148 tu ili aliache eneo hata hivyo akataa vilevile.

“Mara baada ya kuwakatalia niliwaomba nijaze fomu namba 70 ambayo hata hivyo sikupewa hapo ndipo nikaendelea kugundua kuwa kuna njama za makusudi za kutaka kunipora haki yangu,” anasema Mwinchumu.

Anasema mojawapo ya viwanja walivyogawiana ndani ya shamba lake kilichoporwa na watumishi hao ni kiwanja chenye kumbukumbu namba ID -228036 namba 332 chenye eneo la mraba 3,596, Kitalu namba 18 kilichotolewa Septemba 25 mwaka 2014 Kibada Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam.

Mbali na kiwanja hicho, anabainisha viwanja vyake vilivyoporwa ni kama ifuatavyo;

1.   ID 230233 namba 206 kitalu 9 chenye eneo la mraba 56,955, kilichotolewa desemba 2, 2015 Kibada katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam.

2.   ID 228034 namba 327 kitalu 18 chenye eneo la mraba 3,109 kilichotolewa Septemba 25, 2014 Kibada katika wilaya ya Temeke Mkoani Dar es salaam.

3.   ID 228038 namba 335 kitalu 18 chenye eneo la mraba 2,751 kilichotolewa Septemba 25, 2014 Wilayani Temeke Mkoani Dar es salaam na vingine vingi.

4.   ID 228035 namba 329 kitalu 18 chenye eneo la mraba 3,376 kilichotolewa Septemba 25, 2015 Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.

5.   ID 228039 namba 337 kitalu 18 chenye eneo la mraba 1,553 kili chotolewa Septemba 25, 2015 Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.

Mwinchumu anasema katika kuhangaika ili kupata haki yake ameandika barua kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kamishna Mkuu wa Ardhi Tanzania, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mkurugenzi wa Halmashauri ya kigamboni pamoja na Diwani kata ya Kibada bila mafanikio yoyote.

“Hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda alipokuja Kigamboni nilibahatika kumueleza tatizo hili akapiga simu ofisi ya ardhi kanda ya Dar es salaam kwa mtu mmoja anaitwa Nathaniel Mhonge lakini hakuwa na jibu kuhusiana na jambo hili bali alikiri kulifahamu na kujiuma uma tu,” anasema Mwinchumu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kibada Saidi Pazi amekiri kufahamu mgogoro huo na kusema kuwa wanachofanya watendaji hao wa Wizara ni sawa na kuamua kumdhulumu Mzee Mwinchumu haki yake.

Anasema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kunukuliwa akisema kwamba, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne katika kuchangia maendeleo,vitu hivyo ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora..

 Pazi anabainisha kwamba  kutokana na msingi huo wa Mwalimu Nyerere ardhi ni miongoni mwa misingi madhubuti ya Maendeleo ambayo ni haki kwa kila mwananchi kuwa nayo.

 “Hali iliyopo leo ni kinyume kabisa badala ya viongozi wenye dhamana kutuongoza kuitumia ardhi kujikwamua kimaisha imekuwa ni tofauti wanahangaika kuipora toka mikononi wananchi tena kwa kutumia madaraka yao,” anasema Pazi.

Anasema kwamba Mzee Mwinchumu ni mmiliki halali wa eneo hilo ambalo alilirithi kutoka kwa wazazi wake ambao walishaaga dunia, lakini baadhi ya watumishi wa Wizara wamegeuka madalali wa kuuza viwanja hivyo. 

“Kuna haja ya Rais kuiangalia kwa jicho kali Wizara hii kwani kuna baadhi ya watumishi wake sio waaminifu kwasababu badala ya kufanya kazi ya umma wamegeuka kuwa madalali wa kuuza mashamba ya watu kwa kutumia nyadhifa zao,” anasema Pazi.

Anasema mgogoro kati ya Mzee Minchumu na watumishi wa wizara ya ardhi umechukua muda mrefu kwakuwa watuhumiwa ni watumishi wa wizara kila analolifanya mlalamikaji wanahakikisha halifiki sehemu husika huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni kosa.

Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dk. Faustine Ndugulile (CCM) anakiri kuufahamu mgogoro huo na kusema kuwa ni mgogoro wa miaka mingi ambao suluhu yake imekuwa ikikwamishwa na baadhi ya watumishi toka Wizarani wenye maslahi nao.

“Mzee Mwenegowa Mwinchumu amewahi kuja ofisini kwangu kuomba msaada wa suluhu ya tatizo lake lakini limekuwa likikwamia ngazi za juu huko wizarani,” anasema Ndugulile.

Anasema ofisi yake inaandaa utaratibu utakao muwezesha mzee huyo kukutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ili aweze kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kupatiwa haki yake.

Dk. Ndugulile anasema ardhi iliyopo katika maeneo na mipaka ya vijiji kama ilivyoainishwa na taratibu za tawala za wilaya na kisha

kupewa hati ya usajili ya Kijiji huwa ina utaratibu wake wa namna ya kubadili matumizi lakini siyo kwa kuipora toka mikononi mwa wahusika kwa kutumia ubabe.

“Siku zote ardhi imekuwa kisimamiwa kwa mujibu wa taratibu husika ikiwa ni pamoja na sheria ya vijiji ya mwaka 1999 sheria No. 4 ya mwaka 1999 huku ikitoa mwangozo wa jinsi ya serikali kuchukua ardhi toka mikononi mwa wananchi inapotaka kubadilisha matumizi yake sio kufanya kama walivyofanya kwa Mzee Mwinchumu,” anasema Dk. Ndugulile.

Anabainisha kuwa, mamlaka ya serikali za Mitaa zina mamlaka ya kutoa maelezo yoyote yanayohusu ardhi kupitia kamati zake au maafisa wake waliochaguliwa kisheria kwenda kwa Kamishna wa ardhi wa eneo husika lakini juhudi zote hizo zikuwa zikikwamishwa na watendaji wa wizara.

JAMHURI liliwasiliana na Kamishna wa ardhi Kanda ya Dar es salaam Nathaniel Mhonge ili kupata ufafanuzi kuhusiana na madai hayo ambaye amesema kwamba hawezi kuyaongelea kwa madai kuwa  nje ya ofisi yake Mkoani Morogoro kikazi na kumtaka mwandishi kwenda wizarani.

Gazeti hili limefika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweza kupata ufafanuzi kutoka ofisi ya msemaji wa Wizara Mboza Lwandiko aliyetaka kuandikiwa maswali ambayo yalipelekwa kwa Katibu Mkuu.

Lwandiko aliliambia JAMHURI kwamba Katibu Mkuu amesema hawezi kuzungumzia suala hilo, bali anayeweza kuongelea ni Kamishna wa Kanda.

By Jamhuri