📌Ashiriki misa Takatifu Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Daima- Ushirombo

📌Awataka waumini kuweka alama wawapo duniani

📌Atoa wito kumuombea Rais na Serikali kuleta Maendeleo

📌Atoa salamu za mwaka mpya, na kuwataka Watanzania kudumisha Amani na Upendo

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka wazazi nchini kuwajibika kuhusu malezi ya watoto ili kuepusha kuwa na kizazi kisichokuwa na maadili kujenga Taifa imara.

Dkt. Biteko ameyasema hayo leo 31 Disemba, 2023, wakati alipokuwa akitoa salamu za mwisho wa mwaka kwenye ibada ya jumapili katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Daima Ushirombo wilayani Bukombe Mkoa wa Geita.

Dkt. Biteko amesema, wakati tukisherehekea Dominika ya familia, wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ya kulea familia, na ndio maana hata mafundisho ya dini yameelekeza wajibu wa Baba, Mama, na Mtoto kwenye wajibu wa kila mmoja na kudumisha malezi ya familia na Upendo.

“Niwaombe wazazi tuwalee watoto kwenye maadili na kutimiza wajibu wetu ili kuepusha kuwa na kizazi cha walevi, majambazi kwani Jamii kwa sasa haiko vizuri” Alisisitiza Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa jitihada anazofanya kuleta maendeleo kwa wananchi wake na kumshukuru kwa niaba ya wilaya ya Bukombe kwa kuleta Maendeleo na kuifanya kesho ya Bukombe kuwa Bora kuliko ilivyokuwa awali kwenye sekta ya Elimu, na Maendeleo kwa ujumla.

Akiwasilisha salamu za mwaka Mpya Mhe. Dkt. Biteko amewataka Watanzania na waumini kwa ujumla kumfanya japo mmoja kwenye Jamii kuwa mwenye furaha, kudumisha Upendo, Amani na kusisitiza kumuombea Mhe. Rais Samia na Serikali ili kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Paroko wa kanisa hilo Padri Julius Msobi, alimshukuru Mhe. Biteko kwa kushiriki ibada hiyo ya misa Takatifu sanjari na jitihada anazozifanya kuhakikisha wananchi wa Bukombe wananufaika na Maendeleo na kunshukuru Mhe. Rais kwa kuwajali wananchi wa Bukombe.