Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo utakaofanyika Aprili 16-18,2024 jijini Washington DC nchini Marekani.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuimarisha mashirikiano na usimamizi wa misitu ya miombo kwa nchi wanachama za SADC, upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya usimamizi wa misitu ya miombo kwa nchi wanachama wa SADC,namna ya kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda nishati safi pamoja na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mifumo ya ikolojia na uhifadhi wa viumbe hai.

Waziri Kairuki pamoja na ujumbe wake amewasili katika Ofisi za Ubalozi jijini Washington DC na kusaini kitabu cha wageni ambapo katika ujumbe huo ameambatana na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Deusdedith Bwoyo.

Mkutano huo utafanyika chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi na kuhudhuriwa na Mwakilishi wa Wakuu wa Nchi kutoka nchi za SADC pamoja na Mawaziri kutoka nchi za Msumbiji, Namibia na Angola, Wabunge kutoka Malawi, Botswana,Tanzania pamoja na Maafisa Waandamizi katika Sekta ya Misitu wa nchi hizo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (katikati) akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani uliopo jijini Washington DC Aprili 15,2024. Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza (kulia) na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Deusdedith Bwoyo (kushoto).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (kushoto) akijadili jambo  na Balozi wa Tanzania Nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza (kulia) alipowasili katika Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani uliopo jijini Washington DC Aprili 15,2024.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (kushoto) katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza (kulia) alipowasili katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani uliopo jijini Washington DC Aprili 15,2024.

By Jamhuri