Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbarali

MWENYEKITI Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT), Mkoa wa Mbeya na Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kwa utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo ambayo inaendana na thamani ya fedha ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali kwa ajili shughuli mbalimbali ikiwemo elimu ,afya ,maji .

DorMohamed ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Isanga Jijini Mbeya amesema hayo April 15 2024 , wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilayani humo iliyojumuisha wakurugenzi wa halmashauri zote saba za mkoa wa mbeya na baadhi ya wenyeviti wa halmashauri za wilaya pamoja ma madiwani .

Meya Issa amesema miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari Nyeregete, hospitali ya wilaya , ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa halmashauri pamoja na miundo mbinu ya shule ya msingi Ubaruku.

“Mbarali mmeweza kusimamia vizuri miradi hii ya maendeleo ni jambo zuri na halmashauri zingine ziige mfano wa mbarali ili wananchi waweze kuendelea kuwa na imani na serikali yao na kuona kuwa kodi zao zinafanya kazi “amesema Meya.

Lengo la ziara hiyo ambayo imejumuisha na baadhi ya wajumbe wa ALAT mkoa ni kuweza kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali wilayani Mbarali.

Diwani wa Kata ya Rujewa , Jeremiah Makao amesema kuwa miradi hiyo unatekelezwa kwa wakati kutokana na ushirikiano uliopo kati ya madiwani na watumishi samba samba na ushirikishwaji kwa wananchi .

“Hata Mimi kwenye Kata yangu najivunia miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa kwa ubora na ipo imara inaendana na thamani ya fedha halisi hivyo Mbarali tunajivunia kwa kweli na alichozungunza Meya wa Jiji la Mbeya yupo sahihi alichozungumza maana ameona hali halisi ya miradi yetu ilivyo “amesema.

By Jamhuri