Na Paschal Dotto, JamhuriMedia, MAELEZO- Hanang
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutoa huduma muhimu katika maeneo yote yaliyoathiriwa na kuporomoka kwa udongo katika eneo la Katesh Wilayani Hanang mkoani Manyara.
Akizungumza katika mkutano wa Wananchi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepeleka vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha maeneo yote yaliyoathiriwa na maporomoko hayo yanarudi katika hali yake ya kawaida na wananchi kuendelea na shughuli zao.
“Vikosi vyetu vya ulinzi na usalama viko hapa vinaendelea kufuatilia maeneo yote ya milimani na katika kata zote nne hapa Katesh, tunao makamanda 1267 na wote wanafanya kazi hiyo ili kuweka sawa maeneo yote yaliyoharibiwa na maporomoko haya”, alisema Waziri Mkuu.
Mhe. Majaliwa alisema kuwa Serikali inaendelea kuondoa tope na kuzifungua barabara za mji wa Katesh ili shughuli za wananchi ziendelee kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya maporomoko hayo.
Aidha, Majaliwa aliwapa pole wananchi wa eneo hilo na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma bure kwa majeruhi pamoja na wananchi wengine ambao makazi yao yameharibiwa na maporomoko hayo.
“Wananchi wa Katesh na maeneo ya Hanang poleni na kuweni watulivu wakati serikali inaendelea kushughulika na uharibifu huu, nilitaka niwaambie serikali inatoa matibabu bure kwa majeruhi lakini pia huduma za chakula, maji na afya katika makambi yote waliko wananchi wenzetu zinatolewa bure”, alisema Waziri Mkuu.
Pia, Mhe. Majaliwa alisema kuwa viongozi wa serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anawapa pole wananchi hasa wa Katesh ambao wamekumbwa na adha hiyo na kusema eneo lote lililoathiriwa lifanyiwe kazi mapema ili wananchi waendelee na maisha yao ya kawaida.
Aliongeza kuwa watanzania kutoka maeneo mbalimbali wameguswa na wako tayari kuunga mkono kwa michango mbalimbali ili kusaidia waathirika hao ambapo ametoa maelekezo kuwa michango yote ipitie Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa na kufikishwa kwa walengwa moja kwa moja.