Zaeleza ziko tayari kushirikiana na Serikali, Wachimbaji

Dkt. Mwasse Azitoa Hofu Taasisi za Fedha , Aeleza namna STAMICO ilivyosimama Kati

Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia

Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameichambua Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri na kuinadi kwa wadau mbalimbali wa Madini zikiwemo Taasisi za Umma na binafsi zinazojishughulisha na Sekta ya Fedha chini ya Mwamvuli wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kwa kuonesha namna ilivyolenga kukuza uchumi na maisha ya Watu.

Amesema Wizara imekutana na wadau hao ili kujadili mchango wa Sekta ya fedha katika kuinua Sekta ya Madini na kueleza kuwa, sekta hiyo inao mchango mkubwa wa kuiwezesha sekta ya madini kupiga hatua kupitia utoaji mitaji na mikopo ikiwemo kutengeneza nafasi ya ushirikiano ili kuimarisha zaidi Sekta ya Madini nchini.

Ameeleza ikiwa kwa utafiti wa kina wa jiofizikia wa urushaji wa ndege ( high resolution airborne Survey) umefanyika kwa asilimia 16 tu na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) umeiwezesha sekta ya madini kupiga hatua kubwa kiuchumi ikiwemo kuchangia asilimia 56 ya thamani ya bidhaa za madini zilizouzwa nje katika Mwaka wa Fedha 2022/23, hivyo kufanyika kwa utafiti huo zaidi utaongezea tija zaidi.

Akifafanua namna Sekta ya Madini inavyochangia kodi amesema imechangia kodi za ndani kwa asilimia 15 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 2 pamoja na kuchangia Dola za Marekani Bilioni 3.3. kutokana na mauzo ya bidhaa zinazotokana na rasilimali madini kuongeza kuwa ikiwa wizara itawezesha kufanyika kwa utafiti wa angalau kufikia asilimia 50 ifikiapo mwaka 2030 kwa ushirikiano wa taasisi hizo, tafiti hizo zitaliwezesha taifa kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo na kiuchumi kupitia Sekta ya Madini.

‘’Tunataka kufahamu taarifa za miamba, ili tupumike vizuri, hii ndiyo sababu ya dira ya 2030. Ikifika 2030 tuwe tumefanya utafiti kwa nchi yetu kwa angalau asilimia 50. Pamoja na mafanikio hayo bado machango wa sekta ya madini haujakidhi matarajio ya watanzania na taifa letu, zipo changamoto ndiyo sababu tumekutana kupitia kikao hiki kujadili kuwaonesha kilichopo kwenye sekta ya madini, changamoto zilizopo na kutuondoa tulipo,’’ amesema Mhe. Mavunde.

Akizungumzia Madini ni Maisha na utajiri amesema haviwezi kutenganishwa maisha ya mtanzania na Sekta ya Madini na kueleza kuwa kufanikiwa kwa tafiti za kina na kupatikana kwa taarifa za awali, zitachochea sekta nyingine kukua ikiwemo Sekta ya maji na kilimo na kueleza, ‘kilimo wana mkakati wa kuchimba mabwawa 100, kupitia taarifa za GST inaweza kujulikana aina ya maji na hivyo kufanya kilimo chake kwa tija na kuwezesha usalama wa chakula na mapato.

Kuhusu namna Sekta ya Madini inavyoweza kuokoa matumizi ya fedha za kigeni kwa kununua mbolea kutoka nje, amesema zaidi ya tani 350,000 za mbolea zinaagizwa nje kwa kutumia fedha za kigeni kwa ajili ya matumizi ya kupandia, kukuzia na kustawisha , hivyo, taarifa za miamba zitasaidia kujua miamba yenye malighafi zenye mbolea inayohiajika na hivyo kusaidia shughuli za kilimo chenye tija.

‘’ GST imewahi kufanya utafiti wa kina mwaka 2004 kwa kurushwa ndege katika maeneo ya Kahama, Biharamulo, Nachingwea na Mpanda kwa ukubwa wa kilomita za mraba 30,000 tu ikilinganishwa na eneo la ukubwa wa nchi ya Tanzania yenye ukubwa wa kilomita za mraba 945,000 ni kiasi kidogo sana, ndiyo sababu tumekutana na ninyi tuwaeleze fursa ziizopo kwenye Sekta ya Madini , tushirikiane,’’ amesema Waziri Mavunde.

Akizungumzia madini mkakati ameeleza hivi sasa dunia imehamia kuzalisha nishati safi isiyochafua mazingira ambapo madini yanayohitajika kuzalisha nishati hiyo ni pamoja na madini ya graphite, colbat, manganese, nikeli na kueleza kuwa, Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuwa mzalishaji wa madini hayo kwa kuwa yanapatikana nchini na kuongeza , ifikapo mwaka 2050 mahitaji ya madini hayo duniani yatafikia tani milioni 150.

Kufuatia hali hiyo, amesema Sekta ya Madini ni sekta ambayo endapo itafungamanishwa na sekta nyingine itawezesha watu kupata mafanikio, tija, uwekezaji na maendeleo na kueleza kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye utafiti wa madini mkakati.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse wakati akitoa wasilisho amesisitiza kuwa uchimbaji mdogo ni eneo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee na taasisi za fedha na kueleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi Kisheria katika shughuli za uchimbaji mdogo ikiwemo kuliwezesha Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA) kuwa na uwakilishi Tume ya Madini, kuwatengea maeneo na kuwapatia elimu.

Amezieleza changamoto za ukosefu wa masoko, teknolojia duni, kutokukopesheka, elimu, na kueleza kuwa, tayari STAMICO imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuandaa mpango kutoa elimu kwa kuzunguka nchi nzima, kusaini makubaliano na GST kuwezesha kupatikana kwa taarifa za kijilojia, kusaini hati za makubaliano na baadhi za benki ikiwemo CRDB, KCB na NMB na kuelezakuwa, hayo yote yamefanyika ili kupunguza hatari kwa taasisi za fedha na hivyo kuzitaka taasisi hizo kujenga imani na wachimbaji kwa kuwa tayari Serikali imeingilia kati ikiwemo kuwarasimisha.

Ametolea mfano wa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Australia, Down Under na kueleza namna nchi ya Tanzania ilivyokuwa kivutio katika mkutao huo kwenye madini mkakati na kueleza kuwa, taasisi za fedha zinapaswa kutumia fursa za mazingira ya ndani kuwawezesha wachimbaji wadogo kuweza kuchimba madini hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TBA Theobas Sabi amesema anaishukuru Wizara kwa mkutano huo ambao umeziwezesha tasisi za fedha kuielewa Sekta ya Madini, pia amesema kutokuwepo kwa taarifa za kujua kiasi cha madini kilicho kwenye leseni za wachimbaji ni eneo ambalo limekuwa changamoto kwa mabenki na kueleza kuwa, taasisi hizo zitayachukua yaliyozungumzwa katika mkutano huo kwa ajili ya kuyajadili kwenye vikao kazi vya jumuiya hiyo.

Mbali na taasisi za fedha, wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na wafanyabiashara wa madini, watoa huduma, wahimbaji Wadogo, Wa kati Wakubwa. Aidha, wadau hao wamepongeza kwa hatua ya wizara kuitisha kikao hicho.