Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta na wadau wa Maendeleo imeanza Kampeni maalum ya Mkoa kwa mkoa kupambana na vitendo vya ukatili.

Akizungumza wakati wa Kilele cha Kampeni ya kupinga ukeketaji mkoani Manyara Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Wakili Msomi Amon Mpanju amesema Wizara imeamua kuweka nguvu hasa katika kutoa elimu katika ngazi za Mkoa Halmashauri Kata mitaa na vijijini ili kusaidia Jamii kuondokana na vitendo vya ukatili.

Wakili Mpanju ameongeza kuwa kuharibika kwa isingi ya Malezi Bora katika Jamii juu ya suala la Malezi na Makuzi imeelezwa kuwa chanzo cha ukatili ndani ya jamii hivyo Jamii inaoaswa kuzingatia swala la malezi na kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.

Pia Wakili Mpanju ameitaka jamii ya mkoa wa Manyara kuunga mkono jitihada za Serikali na wadau za kupambana na Ukatili wa Ukeketaji nchini kwani wao ni ndio njia pekee ya kuondokana na vitendo hivyo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Wakili Msomi Amon Mpanju akizungumza katika Kilele cha Kampeni maalum ya kupambana na vitendo vya ukeketaji mkoani Manyara.

Ameongeza kuwa Serikali pia inaweka Mkakati katika kuhakikisha Jamii inapata uelewa wa namna kuwalinda Watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili kwa kuanzisha Mwongozo wa Kuunda Madawati ya Ulinzi wa Mtoto shuleni unaosaidia kuwa na sehemu maalum kwa watoto kuripoti viashiria au wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema Mkoa umejipanga thabiti katika kuifukia jamaa na kutoa elimu kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii Maafisa Ustawi wa Jamii ili kujenga uelewa wa madhara na matatizo ya Watoto wa kike kufanyiwa vitendo vya ukeketaji ambavyo ni miongoni mwa vitendo vya ukatili.

“Sisi tunawashukuru Wizara kwa kutuunga mkono katika mapambano haya dhidi ya ukeketaji mkoani hapa sio jambo rahisi sisi tutaendelea kuweka msisitizo katika elimu kwa jamii hasa watoto wa kike na wa kiume ili wawe mabalozi wazuri wa kupambana na Ukeketaji katika jamii” alisemaTwange

Naye Mwakilishi wa Dawati la Jinsia Polisi Makao Makuu Mariam Kipesa amesema Jeshi la Polisi kupitia Dawati hilo imeweka mikakati ya makusudi ili kuhakikisha ukatili hasa ukeketaji unatokomezwa Kawa kuunganisha nguvu ya pamoja baina ya Jeshi hilo wananchi na wadau wengine ili kukiokoa kizazi cha Watoto wa kike nchini.

Kwa upande wake Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara Christopher Olesendeka ameitaka jamii ya Manyara kuendeleaza Kampeni ya kupinga ukeketaji katika Mitaa na vijijini vyao ili kuweza kukabiliana na vitendo hivyo hasa kupata uelewa wafanye nini wanapoona viashiria au kutokea kwa vitendo hivyo vya ukatili hasa ukeketaji.

Aidha Mwakilishi UNFPA Dkt. Majaliwa Marwa amesema Kampeni itakuwa chachu ya kupunguza au kutokomeza vitendo vya ukeketaji na ameishukuru Serikali kwa kuweka Mkakati wa Kutokomeza Ukeketaji kwani inaonyesha dhamira ya Serikali katika kutokomeza ukeketaji na jitihada za kutokomeza ukeketaji zinaanza na msichana mmoja mmoja, jamii na nchi nzima