Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Mohamed Omar, amesema matarajio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona sekta ya kilimo inaleta mageuzi ya kiuchumi nchini.

Amesema kutokana na hatua hiyo ni lazima kufanyia kazi changamoto zilizopo katika sekta ya umwagiliaji ili kuwa na matokeo hayo.

 Amesisitiza kuwa, iwapo serikali haitafanyia kazi mahitaji yaliyopo katika sekta hiyo ya Umwagiliaji hakutakuwa na matokeo katika mageuzi ya kiuchumi yanayotokana na sekta ya kilimo nchini na wizara inaamini utendaji na ufanisi wa Tume unaweza kusimamia na kufikia azma ya Rais ya sekta ya kilimo kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Dkt. Hussein ameyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa Kamati zinazohusika na mradi wa Uhimilivu wa Mifumo ya Chakula unaodhaminiwa na Benki ya Dunia (WB).

 “Mradi huu ni muhimu katika mabadiliko ya tabianchi ili kuwa na usalama wa chakula, hivyo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inalo jukumu mahususi katika kuhakikisha kunakuwa na matokeo chanya katika mradi huu na kufikia maono ya Rais Dk. Samia sekta ya kilimo kuleta mageuzi ya kiuchumi,” amesema.

Naye Mratibu wa mradi huo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Ubora, Naomi Mcharo, akitoa ufafanuzi katika mkutano huo amesema  mradi huo ni wa dola za Marekani milioni 300 na unahusisha Awamu mbili moja wapo ikiwa ni Matokeo Kwanza (P4R) ukiwa ni utekelezaji wa miaka mitano.

Aidha Tume imetengewa Dola milioni 70 kufanikisha mradi huo kipindi hicho.

 “Katika usimamizi na maamuzi ya mradi kunahitaji kuwa na kikao cha wataalamu, Kamati ya watendaji wakuu wa Wizara ambao ni Makatibu Wakuu wa Wizara katika sekta ya kilimo na kikao cha pande mbili za Muungano, lengo ni kuangalia, kushauri na kuelekeza utekelezaji wa mradi ili kuleta ufanisi,” amesema.

Mcharo amesisitiza kuwa NIRC imejipanga kukarabati miundombinu ya umwagiliaji kupitia mradi huo, kuwawezesha na kuwaelimisha wakulima juu ya uendeshaji, matunzo na usimamizi wa skimu za umwagiliaji.