Kutoka katika uvungu wa moyo wangu, nakupongeza kuhutubia mkutano wako wa Arusha  wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, kwa lugha ya Kiswahili ambayo ni ya Taifa lako na umeonesha huna utumwa wa lugha katika maisha yako.

Tumeona mikutano mingi ikifanyika hapa nchini tena ikituhusu Watanzania wenyewe kwa faida yetu wenyewe, lakini ikitumia lugha ya wenzetu ambayo siyo yetu, inakera lakini inatokana na utumwa wa watu wachache.

Uwezo wa mtu yeyote katika utendaji na kuelewa mambo hauna uhusiano na kujua lugha nyingine hasa ya Kiingereza kama ambavyo wengi wametuaminisha katika hili, wachache ambao hatukujifunza lugha hiyo ya Kiingereza lakini tunaelewa mambo kwa kiasi Fulani, tulikuwa tunakwazika sana na mijadala ambayo ni muhimu kwetu lakini hatuielewi.

Rais  Magufuli umetumbua jipu kwa kuwaonesha wasomi ‘uchwara’ kuwa inawezekana kabisa, wanaopaswa kuambiwa ni sisi tuliowengi, na utaratibu wa mikutano ni kwamba wale wachache wasioelewa hupewa wakalimani na huo ndiyo utaratibu wa mikutano yote ya kimataifa inayowahusu wananchi.

Nimefarijika kusikia hotuba ya Arusha, nimefarijika kumsikia kiongozi wangu akitumia lugha yetu kuwasilisha maoni yetu, nimefarijika kwa kuwa ameonesha kuwa Taifa hili lina lugha yake ya Taifa hata kama katika Katiba haitambuliki kama lugha ya Taifa.

Nimefarijika kwa kuwa Rais Magufuli amethibitisha kuwa lugha hii ina uwezo na msamiati wa kutosha katika mawasiliano, nimeridhika na kufurahi kwa sababu sasa tunaweza kuipa heshima lugha ambayo sisi kama Watanzania hatukuipa nafasi kama ambavyo Wakenya walivyoipatia nafasi katika katiba yao kuwa lugha ya taifa.

Lugha hii imechezewa sana na wanaoitwa wanasiasa na wataalamu wa mambo ya kiuchumi na kadhalika, wameidunisha na kuifanya kama lugha ya kienyeji mno, wameshindwa kuithamini kiasi kwamba mtu kuongea Kiswahili ni kama kujidhalilisha katika jamii, kibaya zaidi wakainasibisha lugha ya Kiingereza na usomi wakati siyo kweli.

Katika kuibadili dhana hii potofu nchini, una wajibu wa kujenga imani kwa Watanzania kuwa Kiswahili kinaweza na siyo kweli kwamba Kiingereza ni kila kitu. Unapaswa kusimamia idara zako za Kiswahili ziweze kutekeleza majukumu ya kusimamia lugha hii ili vizazi vya kesho vikumbuke dhima yako katika kuitetea lugha hii. 

Ndugu Rais, kuna mambo mengi yaliyokwama huko nyuma kutokana na vipaumbele, moja kati ya mambo ambayo yalikwamishwa ni pamoja na lugha ya Kiswahili kutumika katika kufundishia. Tafiti zilizofanywa na watu waliobobea katika lugha walithibitisha kuwa mtu hujifunza vyema zaidi kwa kutumia lugha yake.

Kwa bahati isiyo nzuri, suala hili liligeuka kuwa la kisiasa na kuamuliwa kuwa Kiswahili hakiwezi kufundishia, sababu zilizotolewa ni kwamba hakina msamiati wa kujitosheleza na kwamba vitabu na walimu kama vitendea kazi vilikuwa bado havijaandaliwa. Naomba huu uwe mtihani kwako kuuthibitishia ulimwengu kuwa hili linawezekana, iwe hapa kazi tu kwa kuandaa kile kilichoelezwa kuwa kipo nje ya uwezo wetu na kwamba kuna sababu zilizo nje ya upeo wetu.

Rais Magufuli tukumbuke kuwa nchi za wenzetu zilizopiga hatua mbalimbali za kiuchumi zinatumia lugha zao. Iangalie China ambayo tulizaliwa wote tukiwa maskini lakini leo wapo wapi? Ureno, Ujerumani, Ufaransa na nchi za Scandinavia je?

Lugha ni biashara kubwa sana duniani, Waingereza wanaishi kwa kutumia lugha yao, wanaitumia kuinua uchumi wao pasi na sisi kutoelewa, wanazalisha walimu, vitabu, uelewa na lojistiki mbalimbali za kidiplomasia katika kujiingizia kipato kwa kutumia lugha, wanatumia lugha katika kubadili utamaduni wa nchi maskini ambazo zimekubali kuwa watumwa wa lugha yao.

Nimesema umeanza vizuri, umetufurahisha sisi wachache ambao tunaelewa heshima na utu wa mtu katika kuthamini kilicho chake, wapo watakao jenga hoja za kipuuzi na kuona kama hukutoa hotuba nzuri kwa sababu ulitumia Kiswahili, wapo watakaoona kama ulitudunisha kwa kutumia lugha yetu, hawa ndiyo wale wanaoendelea kutawaliwa na fikra potofu za kuamini msomi ni yule anayejua Kiingereza.

Naomba uthibitishe kuwa suala la lugha linawezekana, na hata ukienda katika mikutano ya kimataifa huko ughaibuni tafadhali naomba ukatumie Kiswahili kukandamiza hotuba yako, wakalimani wapo huko watafanya kazi yao na hapo utakuwa umetoa ajira kwa Watanzania watakaofanya ukalimani.

Sitaki kukwambia mengi lakini nikuthibitishie kuwa sisi tulio wengi tumekubariki na tunashukuru kwa kuonesha kuwa hata hili limewezekana. Hapa kazi tu.

 

Wasaalam, 

Mzee Zuzu

Kipatimo

1176 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!