YAH: SIMULIZI YA TANZANIA NIIJUAYO

Sijasimulia kiasi cha kutosha juu ya nchi yangu niipendayo, nchi ambayo nimeiishi kwa maisha na matendo, nchi ambayo ninaijua ‘ndani nje’, iwe kiuchumi, siasa, utamaduni, teknolojia, uzalendo na zaidi ya yote kiuongozi.

Ni nchi ambayo labda inaweza ikawa ni historia kwa nchi nyingine kama wakiwa waungwana wa kukumbuka fadhila za ujirani mwema.

Wapo ambao wanaijua vizuri nchi yangu, na wapo wanaofikiri wanaijua nchi yangu na wapo ambao hawaijui nchii hii. Lengo la waraka huu ni kwa wale wasioijua kabisa nchi hii.

Nimepata bahati ya kukutana na vijana wengi ambao hasa kimsingi ndiyo tutakaowakabidhi Taifa letu, na nimebaini wana uelewa mdogo kuhusu msingi wa mada hii.

Hawa ndiyo nimewalenga ili wajue kitu kinachoitwa historia ya nchi yetu, leo nitagusa misimamo michache ya awamu zote tano.

Itakuwa kama ninaonja ladha ya jambo lakini ukitaka kulila, huna budi kutafuta maandiko na kumbukumbu za kweli katika haya na yale ambayo sitayagusia.

Awamu ya kwanza kabisa, uongozi ulikuwa wito, awamu ya kwanza ndipo ilipokuwa chimbuko la imani ya chama kwenda sanjari na imani za kidini, ni kipindi hicho ndipo tulisema kutoitendea haki nchi yetu ni dhambi na siyo kosa la jinai au uhujumu uchumi.

Kiongozi aliapa kwa kuilinda Katiba kama jambo la kiroho. Awamu ya kwanza hakukuwa na siasa za kujitafutia umaarufu, awamu ya kwanza ambayo kimsingi ndiyo awamu ya uzazi wa vijana na wazee wa leo haikuwa na umaarufu wa kufanya mambo ya vituko na kujulikana.

Awamu ile mtu alikuwa maarufu kwa kilimo chake, mashamba yake, mifugo yake na uongozi wake, ni awamu ambayo kila mtu alitamani awe kama mtu maarufu kwa kufanya kazi kwa bidii na kujitolea.

Awamu ya kwanza, watu waliamini katika uhuru wa kufanya kazi na siyo uhuru wa kukaa bila kufanya kazi.

Awamu ya kwanza tuliamini katika siasa ya kufanya kazi na siyo siasa ya kukaa katika majukwaa, hii ndiyo nchi ninayoikumbuka.

Awamu ya kwanza ilifuta ubaguzi na kuleta usawa, awamu ya kwanza ilikuwa ya Tanzania yetu na kila Mtanzania kuwa askari wa nchi yake.

Najaribu kugusia tu kidogokidogo, awamu ya pili ilikuwa wakati wa mageuzi ya kiuchumi duniani, nchi yangu iko duniani ilikumbwa na kadhia hiyo.

Kwa uzalendo wetu tulikubali baadhi ya mambo yaingie ili tuweze kwenda na dunia mpya.

Ni awamu hii ndipo tulipovamiwa na mdororo wa kiuchumi na kuruhusu mfumuko wa bei, mabepari walianza kuinyemelea nchi yetu na kumea ndani ya nchi.

Ninakumbuka mambo mengi yaliyoyumbisha uchumi wetu ikiwamo madeni makubwa ambayo nchi hii ilikuwa nayo kutokana na ukombozi wa nchi mbalimbali kusini mwa Jangwa la Sahara.

Awamu hii tulifungua milango ya biashara kwa lazima na kusababisha kufa kwa viwanda vingi ambavyo labda kama vingelikuwapo, basi Tanzania ya viwanda tunayoimba leo ingekuwa mbali.

Awamu hiyo ndipo imani na maisha yalipoanza kubadilika kutoka katika kuwajibika na kuwa wafanyabiashara wa maneno na bidhaa, ni awamu ngumu kuikumbuka kutokana na ajira nyingi kwisha na kuwaacha Watanzania wengi mitaani bila kazi.

Lakini pia wakulima wa mazao ya biashara kushindwa kuwa na soko la bidhaa zao.

Kama Taifa tulipigana na kuhakikisha kuwa haturudi kuwa watumwa wa wenye mali na kamwe hatuwezi kuuzu utu wetu kwa sababu tu ya mfumo mpya wa mabadilliko ya kiuchumi duniani. Nawaandikia msiojua historia ya nchi yetu.

Ikaja awamu ya tatu, awamu ambayo ilipokea mzigo mzito wa awamu ya pili, ni awamu ambayo kimsingi nchi nyingi za Afrika zilitegemea uamuzi wa nchi za Ulaya.

Tanzania ilikuwa moja ya nchi zilizokuwa na kiburi cha kukataa kutawaliwa, lakini ndiyo wakati ambao mataifa makubwa ya Ulaya yalihanikiza siasa na utamaduni wao katika mataifa ya Afrika.

Ni kipindi ambacho baadhi ya Watanzania walitumika kuibomoa nchi yao, walianza kuthibitisha kwamba yale maradhi ya kwisha kwa uzalendo yanaanza kuwa sugu, ni kipindi ambacho uongozi ulikuwa na wakati mgumu kuirudisha nchi katika mfumo wake wa siasa, utamaduni na kadhalika.

Tuombe Mungu iendelee wiki ijayo

Wasaalam

Mzee Zuzu

Kipatimo.