NA MICHAEL SARUNGI

Mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha ubora wa viwanja kabla ya timu kuruhusiwa kutumia viwanja hivyo ili kudhibiti fujo na kuepusha matatizo yanayoweza kutokea kati ya washabiki na wachezaji.

Wakizungumza na JAMHURI, baadhi ya wapenzi wa michezo nchini wamesema wachezaji ni wanadamu kama walivyo wengine, wanaoweza kupandwa na hasira na kujikuta wakitenda vitendo visivyotakiwa michezoni.

Ernest Bujiku, bondia mstaafu wa uzito wa kati nchini, amesema kuna haja ya suala la nidhamu kuangaliwa kwa upana zaidi kuliko ilivyo sasa, ambako mchezaji ndiye anayeonekana kuwa na utovu wa nidhamu panapotokea matatizo.

Nimesikia kupitia vyombo vya habari suala la beki wa Kagera Sugar, Juma Nyoso, akituhumiwa kumpiga shabiki aliyemfuata uwanjani kumzomea hili si jambo zuri, lakini tujiulize shabiki alifikaje uwanjani,” amesema Bujiku.

Amesema shabiki anaweza akaruhusiwa kumzomea mchezaji anapokuwa jukwaani, lakini inapofikia hatua ya shabiki kumfuata mchezaji ndani ya uwanja na kuanza kutukana ni jambo lisilokubalika katika mchezo wowote.

Suala la nidhamu michezoni linapaswa kuangazia pande zote ndiyo maana tumekuwa tukisikia mashabiki wakifungiwa kuhudhuria katika michezo mbalimbali kwa makosa kama haya,” amesema Bujiku.

Amesema ifike wakati mashabiki nao wajiheshimu kuliko kuona kuwa wenyewe wako sawa kutenda lolote kwa mchezaji hata kama jambo hilo linaweza kuwa la maudhi kwa mchezaji awapo ndani au nje ya uwanja.

Mohamed Hussein, mchezaji wa zamani wa Klabu ya Yanga na Timu ya Taifa (Taifa Stars), amesema suala la kudumisha nidhamu uwanjani linapaswa kuangaliwa kwa upana zaidi kuliko kulisisitiza kwa wachezaji pekee.

Ni kweli nidhamu ni muhimu kwa wachezaji, lakini kuna mengi ya kujiuliza ilikuwaje shabiki akaingia uwanjani huku kukiwa na ulinzi wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine, hapa lazima kuna mengi ya kujiuliza,” amesema Hussein.

Amesema kuna haja kwa mamlaka zinazohusika kujiuliza maswali kama vinatekeleza majukumu yao ipasavyo wakati wa michezo nchini kama jibu ni ndiyo au hapana?

Amesema nidhamu ni muhimu kuwapo kwa kila mpenda michezo bila ubaguzi  na kuongeza kuwa hilo likiwezekana kila kitu kinaweza kuwa salama kuliko watu walivyokariri sasa kuwa anayepaswa kuwa na nidhamu ni mchezaji pekee.

Amri Kiemba, mchezaji wa zamani wa Klabu ya Simba, ameshauri kuwa twendako kuna haja ya michezo nchini kuwa na wataalamu wa saikolojia ili kupunguza vitendo ambavyo si vya kimichezo vinavyoweza kufanywa na wachezaji na mashabiki.

Kama mtu ameandaliwa vizuri kisaikolojia anakuwa na uwezo wa kukabiliana nalo, sisi mpira tunacheza tu lakini kitu ambacho kina mambo mengi nyuma yake, mchezaji anatakiwa kupewa maandalizi muhimu kisaikolojia kabla ya kuingia uwanjani,” amesema.

Amesema wakati mwingine hata wachezaji wa Ulaya inatokea wakashindwa kuhimili maneno ya mashabiki; mfano mchezaji Patrice Evra mwaka jana alimpiga teke shabiki baada ya kukerwa na matamshi aliyokuwa akitolewa na shabiki huyo.

mwisho

Please follow and like us:
Pin Share