DAR ES SALAAM

NA CLEMENT MAGEMBE

Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) umehimiza matumizi sahihi ya alama zinazoonesha barabara za mchepuko kwa magari yanayopita makutano ya barabara za Nyerere na Mandela, ili kuepuka foleni zinazoweza kuzuilika.

Makutano hayo ndipo panapojengwa barabara ya kupita juu maarufu kama Tazara fly over, lengo likiwa ni kupunguza foleni za magari hususani yanayopita kwenye barabara hizo.

Kutokana na ujenzi huo, eneo la barabara ya Nyerere kuanzia Tazara hadi Vingunguti na kutokea hapo kuelekea mjini hadi maeneo ya Mtava, pamekuwa na msongamano unaosababishwa na foleni ndefu.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Julius Ndyamukama, amelieleza JAMHURI kuwa tatizo la foleni kwenye maeneo hayo linasababishwa na madereva kutofuata maelekezo ya namna bora ya kutumia barabara za mchepuko, ili kuvuka kwa urahisi makutano hayo.

Ndyamukama amesema madereva wamekuwa wakivuka njia za mchepuko na wanapokaribia eneo la ujenzi, wanashindwa kurudi nyuma ili kupita kwenye barabara za mchepuko.

Hii imekuwa changamoto kubwa, alama zipo lakini madereva wanashindwa kuzifuata, tunakusudia kuwaelimisha zaidi ili waelewe namna ya kutumia njia zilizopo katika eneo hilo,” amesema Ndyamukama.

Amesema Tanroads inatarajia kutoa matangazo zaidi kwa njia za michoro na maandishi, ili kuwaelimisha watumiaji wa barabara na kudhibiti foleni kwenye barabara hizo.

Wiki iliyopita, baadhi ya watumiaji wa barabara hizo walilalamikia uwepo wa foleni kubwa za magari katika makutano hayo, hivyo kusababisha wachelewe kufika katika shughuli zao.

Mkazi wa eneo la Banana jijini Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina la Maulidi Ramadhan, amesema foleni za magari katika eneo hilo zinawaathiri ikiwamo kupunguza ufanisi katika shughuli za kiuchumi.

Kila siku napita hapa Tazara, lakini foleni za magari tunayotumia zimekuwa kero mno kwani tunachukua muda mrefu sana barabarani na kuchelewa katika shughuli za kiuchumi,” amesema Ramadhan.

Akikagua ujenzi huo, Agosti mwaka jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu, ili kuanza kutumika na wananchi ikiwa ni azma ya Serikali ya kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.

Mradi wa ujenzi huo umefadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), na hadi kukamilika kwake utagharimu Sh bilioni 99.

Mwisho

By Jamhuri