Mara nyingi huwa najaribu kufanya tathmini yangu ya kazi ambazo natakiwa kuzifanya kutokana na kuaminiwa na wenzangu, inaweza ikawa ushenga, ushereheshaji, kufanya utambulisho, kusoma hotuba au risala na kadhalika.

Inapotokea ukapewa heshima hiyo, unatakiwa kuheshimu kazi na kuwaheshimu waliokupatia kazi, unatakiwa kujali na kuthamini heshima hiyo kwa nafasi hiyo uliyopewa kwa imani ya waliokuteua. 
Nakumbuka zamani ilikuwa tunafanya uchaguzi wa viongozi wetu kwa kuangalia hekima, busara na kujituma kwa mtu mwenyewe, vigezo vya shule havikuwa na maana sana kwa sababu hatukuamini kuwa shule peke yake ingeweza kukidhi haja ya busara, heshima na hekima. 
Tuliowachagua walilijua hilo, na walitumia nafasi hizo kwa heshima kubwa kwa sababu walijua ni hekima na busara za waliochagua kuangalia vigezo ambavyo wengine walikuwa wamepungukiwa navyo. 
Hivi sasa kuna kazi nyingi za kufanya kwa niaba, lakini pia kuna kazi nyingi ambazo lazima tuchaguane kwa vigezo hivyo hivyo ili mmoja awe ndiye kiongozi wetu na wengine tumsikilize yeye. 
Katika miaka ya hivi karibuni, kumetokea kundi la watu waliodai kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hizo kwa niaba, kama kuwa mshereheshaji au master of ceremony (mc). Wapo waliojigawa kwa makundi kwamba kuna washereheshaji wa harusi, ngoma za mwali, vigodoro, mikutano, sherehe za kitaifa na kadhalika. 
Walijigawa kutokana na taaluma yao walioisomea japo sina hakika kama ushereheshaji unasomewa au ni taaluma na siyo kipaji, walijigawa kutokana na kazi zao na jinsi walivyo, kwa utanashati na kumudu makundi wanayofanyia kazi. 
Leo nimeamua kuzungumzia hili kwa sababu kubwa moja, kwamba baadhi yao hao tunawapa kazi hizi kwa heshima lakini  wao hugeuka na kuamua kuharibu shughuli zetu kwa kukosa heshima katika majukumu yao. 
Kuna shughuli ambazo kamwe hazirudiwi, ikifanyika ni mara moja na hakuna kumbukumbu ya kuifanya tena. Mathalani siku chache zilizopita tulikuwa na sherehe kubwa ya kutimiza miaka 50 ya Uhuru. Tulikuwa watu wengi na tulihitaji mtu mmoja awe msemaji ili tuelewe kinachoendelea, watu wale wachache tuliowachagua walifanya kazi yao vizuri na waliiheshimu kazi yao kutokana na jinsi ambavyo wao waliona tumewapa nafasi hiyo kwa heshima tu. 
Kwa bahati mbaya, hivi sasa na hasa ninyi vijana wa dot.com, hamtaki kuheshimu kazi wala madaraka ambayo tumeamua kuwapa mfanye kwa niaba yetu, wapo wanaodiriki hata kuropoka matusi huku wakijua tuliopo mbele yao tuna umri tofauti na wao na pengine tuna nasaba na hao tulionao. 
Kuna shughuli ambazo hazihitaji kuchekesha bali zinahitaji kuvuta hisia za watu, kuna shughuli makini za watu makini na tunatakiwa kujua sisi ambao tumeombwa kufanya shughuli hiyo kuwa makini. 
Kwa bahati mbaya sasa hivi umakini na shughuli hizi haupo, inawezekana ni kwenda na wakati, lakini suala la kuheshimu shughuli tuliyopewa lipo palepale. Leo hii shughuli ya kitaifa iliyokusanya watu tofauti na uhusiano tofauti inaweza ukawa uwanja wa matusi na baadhi ya waandaaji wakafurahia tukio hilo, bila kujua limewakwaza watu wengine kwa kiwango gani. 
Sasa hivi hakuna heshima kama zamani ya kumuomba mtu afanye jambo kwa niaba yetu wengi, heshima tumeiweka rehani, mwongozaji wa shughuli anaweza kutumia fursa hiyo kumaliza hasira zake kwa matusi ya nguoni mbele ya kadamnasi anayoiongoza. 
Tuheshimu kazi tunazopewa na tuzipe thamani kazi hizo, kama ni shughuli ya kigodoro basi tujue kuwa kuna watoto wamelala maeneo hayo, kama ni harusi basi tujue kuna wakwe katika tukio hilo, kama ni mhadhara basi tujue kuna wasomi na watu wazima mahala hapo, kama ni tamasha basi tujue watu wana itikadi tofauti na kadhalika. 
Tujue kuwa sauti zetu zinasafiri, utani unaweza kuvunja ndoa, uchumba, undugu, urafiki, na kushusha heshima ya mtu mbele ya jamii, lakini pia hata sisi tunaowachagua wasemaji wetu tufanye tathmini ya kutosha na kujua kama shughuli yetu ni ya kihuni ama ya heshima. 
Imenikera sana shughuli ya watu siku za hivi karibuni ilipovamiwa na dot.com na kugeuza ukumbi kuwa uwanja wa matusi, kushushiana heshima, kuropoka ovyo wakati jambo linalofanyika linaitwa la kitaifa.

Wasaalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.

By Jamhuri