Home Michezo YANGA YATINGA NUSU FAINAL KOMBE LA MAPINDUZI, YAIFUNGA TAIFA 2-0

YANGA YATINGA NUSU FAINAL KOMBE LA MAPINDUZI, YAIFUNGA TAIFA 2-0

by Jamhuri

Ajibu ameisaidia Yanga kupata ushindi wa mabao 2-0, na kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi

Miamba ya soka Tanzania Bara, Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya timu ya Taifa ya Jang’ombe na kuungana na Singida United pia kutoka kundi A, kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2018.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi tisa sawa na Singida United lakini yenyewe ikiwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga ukilinganisha na Yanga ambayo inamabao matatu pekee.

Matokeo hayo yanazitoa timu za Mlandege, JKU na Zimamoto katika harakati zote za Zanzibar kutokana na uchache wa pointi waliokuwa nao kwenye kundi hili ambalo lilikuwa linaundwa na timu tano.

Ibrahim Ajibu alianza kuifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya 45, baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Jangombe Boyz Ahmed Seleman, kufuatia shuti kali la Yohana Nkomola.

Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao hilo huku wapinzani wao Jangombe licha ya kuumiliki sana mpira lakini waliweza kufanya shambulizi moja katika kipindi cha kwanza  dakika ya 29 ambapo shuti la Yussufu Joseph lilipanguliwa kiufundi na kipa chipukizi wa Yanga Ramadhani Kabwili.

Kipindi cha pili Jangombe Boyz walikianza kwa kasi na kushuhudia Yanga wakicheza kwa kujihami zaidi huku wakitumia mashambulizi ya kustukiza lakini wapinzani wao walishindwa kuitumia nafasi hiyo kupata bao.

Dakika ya 60 Nkomola aliifungia Yanga bao la pili baada ya kupokea pasi safi ya Ajibu akiwa ndani ya eneo la hatari ambapo shuti hilo lilimshinda kipa Juma Machano, aliyeingia muda mfupi tangu kipindi cha pili kuanza akichukua nafasi ya Seleman aliyeumia.

Bao la Nkomola lilionekana kuizindua Yanga na kuendelea kufanya mashambulizi makali kwenye lango la Jang’ombe Boyz na dakika ya 64 Rafael Daud alipoteza nafasi ya wazi kufuatia kipa Machano kupangua mpira alioupiga kiungo huyo akiwa ndani ya eneo la hatari baada ua kupokea pasi nzuri ya said Mussa.

katika dakika za mwisho kocha wa Yanga Shedrack Nsajigwa aliwapumzisha wachezaji Daud, Nkomola na Geofrey Mwashiuna na nafasi zao kuchukuliwa na Yusufu Mhilu, Pius Buswita na Juma Mahadhi ambao walionekana kuuchangamsha mchezo huku wapinzani wao wakionekana kukata tamaa kutokana na muda uliobaki.

Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga Ibrahim Ajibu alichaguliwa kuwa mchezaji bora katika mechi hiyo kutokana na kuonyesha kiwango bora na kutengeneza nafasi nyingi kwa wachezaji wenzake.

Yanga imebakiwa na michezo miwili dhidi ya Zimamoto na Singida United ambayo ndiyo itaamua kati yao au Singida United nani anakuwa wakwanza kwenye kundi lao.

You may also like