Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amesema Zanzibar inatarajia kunufaika na Biashara ya Kaboni wakati wowote kuanza sasa.
Amesema hayo leo Juni 13, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azan Mwinyi.
Mhe. Khamis amesema ili kutekeleza suala hilo, watalamu wapo katika hatua za mwisho za kufanya utafiti kwenye maeneo yenye misitu ya asili upande wa Tanzania Zanzibar.
Ameitaja Msitu wa Jozani uliopo Unguja na Ngezi katika Kisiwa cha Pemba kuwa inaweza kutumika kuvuna hewa ya ukaa na kuwapatia faida wananchi wa visiwani humo.
Kuhusu kuwapa uelewa wananchi, Naibu Waziri amebainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar inatarajia kutoa elimu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
“Mheshimiwa Naibu Spika utakumbuka pia juzi tumetoa semina kwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Maji na Mazingira pamoja na ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu hewa ya ukaa ili kuwanjengea uelewa,” amesisitiza.
Amesema kuwa Serikali imeunda kikosi kazi kilichoshirikisha Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ambacho kinazunguka nchi nzima kutoa elimu kuhusu hewa ya ukaa hususan katika mikoa ya Tabora, Simiyu, Katavi na Manyara, Katavi na maeneo mengine.
Hivyo, amesema kuwa Serikali imeweka mipango thabiti ya kusimamia na kutathmini biashara hiyo ambapo imetoa mamlaka kwa Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kilichopo mjini Morogoro ambacho kinaratibu na kutoa utaalamu kuhusu gesijoto nchini.
Sambamba na hilo pia imeandaa Kanuni na Mwongozo wa mwaka 2022 kwa ajili ya kusimamia biashara na kuhakikisha inakuwa rasmi kwa wadau ili iwanufaishe na kusaidia katikia utunzaji wa mazingira.