Na Albano Midelo,JamhuriMedia,Ruvuma

Takwimu za uzalishaji wa zao la korosho mkoani Ruvuma zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano mfululizo zao hilo limewaingizia wakulima shilingi bilioni 291.9.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anafungua mkutano wa wadau wa korosho uliofanyika kwenye ukumbi wa Cluster mjini Tunduru.

Amesema kuanzia msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 hadi kufikia msimu wa mwaka2021/2022 wakulima walivuna jumla ya kilo za korosho 104,819,739 zilizouzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 2,802 na kuwapatia wakulima mabilioni ya fedha.Hata hivyo Kanali Thomas amesema katika msimu wa mwaka 2021/2022 pekee, Mkoa wa Ruvuma ulikusanya jumla ya kilo 25,284,493 za korosho zenye thamani ya shilingi bilioni 50.6 ambazo zimeuzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 1,971.60 kwa kilo.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas

“Katika kuendeleza zao la korosho juhudi nyingi zimefanywa na serikali na wadau wa korosho,katika msimu wa mwaka 2021/2022 kilo 7,183 za mbegu za korosho zilisambazwa kwa wakulima,kilo 1,569,525 za viuatilifu vya salfa ya unga na viuatilifu vya maji lita 89,717 vilisambazwa kwa wakulima’’,alisema RC Thomas.

Mkutano huo umewezesha kufungua msimu wa masoko wa 2022/2023 ambapo Mkoa wa Ruvuma umejiwekea malengo ya kuzalisha tani 32,069,501 za korosho na kuwezesha kuchangia lengo la kitaifa la kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi na kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025/2026.

Baadhi ya maghala katika Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru TMCU ambayo yanatumika kuhifadhia mazao yanayouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambayo ni korosho,mbaazi na soya.

Mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tatu kitaifa katika uzalishaji wa zao la korosho,ukiongozwa na mikoa ya Mtwara na Lindi