Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mbunge wa Ilala na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amewataka Watanzania kuendelea kulipa kwani ni muhimu kwa maendeleo ya Nchi.

Amesema lengo kuu la serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuondoa utegemezi kwa mataifa mengine na kujivunia maendeleo ya Nchi kwa kulipa kodi.

Zungu ameyasema hayo leo Machi 16, 2024 katika semina iliyotolewa kwa viongozi wa chama hicho katika Jimbo la Ilala yenye mada tatu ambazo ni umuhimu wa watanzania kulipa kodi, uchafuzi wa mazingira ambao unaathiri uchumi wa bluu pamoja na Uwekezaji.

“Ni muhimu sana kulipa kodi…leo Watanzania tuko mil 61, hivyo bila kodi na uwekezaji mkubwa hatuwezi kusaidia katika kupata huduma bora. Tuwaombe viongozi wetu mnapokwenda kutoa somo hili lazima muwatahadharishe wafanyabiashara kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanajua kila kitu, msipotoa risiti wanajua na ukitoa wanajua.

“Tumeamua kufanya semina hii kwa viongozi wetu ambao ndio wanaishi na watu huko, hivyo wataweza kusaidia kueleza umuhimu wa kulipa kodi, kutunza mazingira na masuala ya uwekezaji. Viongozi hawa ambao wako hapa wapo kwenye mitaa yote ya jimbo hili la Ilala ambalo ndilo walipaji wakubwa wa kodi,” amesema Zungu.

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Ilala, Said Sultan amesema viongozi hao wana wajibu mkubwa wa kuhimiza na kushawishi wananchi kulipa kodi.

“Kama mnavyofahamu Jimbo la Ilala ndio hub ama kivuko kwa serikali katika kukusanya kodi. Hivyo viongozi wa Chama katika Jimbo letu wanaowajibu mkubwa wa kupata elimu hii kwa faida ya kulipa kodi, kwanza itawasaidia wenyewe walipe kodi pamoja na kuwaambia wananchi…lakini kubwa zaidi kujenga utaratibu wa kutoa na kudai risiti. TRA wametuambia wana mfumo kule kwao ambao mtu ukitoa risiti kule mfumo unasoma hii inawasaidia katika kukusanya taarifa,” amesema Said.

Naye Afisa Msimamizi wa Kodi Mkuu kutoka TRA, Hamad Mterry amesema wameamua kutumia fursa hiyo kama jukwaa la kutoa elimu kwa walipa kodi ambapo wanaamini kupitia viongozi hao ujumbe utawafikia wananchi wengi.

“Hafla hii ina viongozi wa CCM takribani 900 kwa hiyo tunaamini tukiwafikishia hawa elimu wana watu wengi ambao wako nyuma yao hivyo tunakuwa tumefikisha elimu hii ya mlipa kodi kwa watu wengi.

“Na kipindi hiki cha mwezi wa tatu ndo TRA tunafanya makadirio ya kodi ambayo mtu atalipa mwaka mzima kwa awamu nne tofauti. Kwahiyo imekuwa ni siku muafaka ili wakapeleke elimu na kuhamasisha wafanyabiashara waliopo katika maeneo yao kwa pamoja waweze kufika katika ofisi zetu kwaajili ya makadirio,” amesema Mterry.

Amefafanua kuwa, pia wameamua kutumia jukwaa hilo kuendeleza kampeni ya kuwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kudai rsiti na yule anayehudumia atoe risiti.

“Kwasababu unapofanya hivyo yale mauzo yanakuwa yamerekodiwa kupitia mfumo wetu na hata mfanyabiashara akiyaficha mauzo yake sisi tayari tunakuwa nayo. Pia tumewafafanulia umuhimu wa kulipa kodi ambapo tumewaeleza bajeti ya serikali ni Sh. Trilioni 44 na kati ya hizo, Trilioni 26 zinatakiwa kutolewa na TRA ambayo ni sawa na asilimia 60.2 ya bajeti yote ya serikali,
kwahiyo mtaona ambavyo TRA tuna jukumu zito la kuchangia bajeti ya serikali, hivyo tunawasihi wananchi na wafanyabiashara muwe na moyo wa kulipa kodi kwa hiari.

“Vilevile, tunawaomba mtoe taarifa kwa wanaokwepa kodi, na hizi taarifa zinalipa kwani endapo utafanikisha kutoa taarifa utapatiea asilimia tatu ya kodi iliyokombolewa ambayo kiwango cha mwisho ni Sh milioni 20,” amesema Mterry.

By Jamhuri