Na Mwandishi Wetu
 
Bohari ya Dawa nchini (MSD) katika kuongeza unfanisi na kufikisha huduma karibu na wananchi katika mwaka huu wa fedha imepanga kuzindua bohari za kisasa za kuhifadhia dawa katika mikoa ya Kagera na Ruvuma.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu amesema katika mahojiano kuwa hatua hiyo inalenga kusogeza huduma ya dawa karibu na wananchi hivyo kuchangia kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015 kwa vitendo inayotaka kuwa na taifa la watu wenye afya njema.
Amesema ujenzi huu utafanyika Bukoba Mjini katika eneo la Kata ya Nyanga, ambapo Bohari itakuwa na eneo lenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 5,000 na hivyo kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Kwa sasa Kagera inahudumiwa na Kanda ya Mwanza, kupitia Kituo cha Mauzo (sales point) cha Muleba, ambacho ni kidogo na miundombinu yake haikutengenezwa kwa ajili ya bohari ya kuhifadhi dawa. Tunaishukuru Halmashauri ya Mji wa Bukoba, imetupatia eneo zuri, lipo karibu na mji na kijiografia litaiwezesha MSD kusambaza dawa kwa urahisi kwenda maneo yote ya Mkoa wa Kagera. Kagera tunaifanya Kanda sasa na eneo lilipo miundombinu inayolizunguka ni mizuri, ikiwamo barabara ya lami,” amesema Bwanakunu.
Amesema kwa sasa Kanda ya Mwanza inahudumia mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza yenyewe, Mara, Shinyanga na Simiyu. Kwa kutilia maanani kuwa Kanda ya Ziwa ina theluthi moja ya Watanzania, kwa mujibu wa senda ya watu na makazi ya mwaka 2012, MSD imeona ni busara kuongeza bohari mkoani Kagera kurahisisha usambazaji wa dawa.
Uamuzi wa kuwa na Kanda ya Kagera ya MSD ulifikiwa mwaka 2014 na Muleba ilijitolea kutoa majengo yaliyokuwa yamejengwa kwa ajili ya hospitali yatumike kuhifadhi dawa kwa muda, huku ikizihudumia pia wilaya za Mbogwe na Bukombe za Mkoa wa Geita, ambapo sasa wilaya zote hizo zitahudumiwa rasmi na Kanda ya Bukoba. Bohari hii itazihudumia wilaya za Bukoba (M), Bukoba (V), Msenyi, Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Muleba.
Wakati wanaanza kituo cha Muleba kilikuwa na wateja 250, ila kwa sasa wamefikia wateja 338, kwa maana ya hospitali na vituo vya afya. Walianza na eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 250, lakini sasa hivi wana mita za mraba 500 na hazitoshi. Wafanyakazi walikuwa watatu na sasa wako 15. Kwa kuanzia bohari itakuwa na mita za mraba 2,500 ila ujenzi ukikamilika zitakuwa mita za mraba 5,000 pale Nyanga Bukoba. Halmashauri ya Mji imewapatia ekari 7.
Kwa sasa MSD wanasema upatikanaji wa dawa wanazozifuatilia 135 ni asilimia 90 katika vituo vyote vya afya nchini, zahanati na hospitali za ngazi mbalimbali. Kituo cha Nyanga Bukoba kikikamilika Kanda ya Bukoba itapewa magari 11 mapya ya kusambaza dawa. Kituo hiki kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwakani.
MSD inahudumia zahanati, vituo vya afya, hospitali, hospitali teule za wilaya, hospitali za wilaya, hospitali za mkoa na hospitali za rufaa nchini. Kimsingi Kanda moja inapaswa kuhudumia mikoa miwili, hivyo kujengwa kwa bohari ya Bukoba kutakuwa kumeipunguzia mzigo Bohari ya Mwanza ambayo tayari ina kazi kubwa.
Taarifa zinaonyesha kuwa Mkoa wa Kagera na mikoa yote inayozunguka Ziwa Victoria, ina kiwango cha juu cha malaria na magonjwa ambukizi, ambapo kwa sasa dawa zinazotumika kwa kasi kubwa ni ARVs, za malaria, TB na dawa za maumivu.
“Kimsingi tunamshukuru Mhe. Rais John Magufuli kwa kuongeza bajeti ya dawa nchini. Sisi huwa tunapima upatikanaji wa dawa kwa wananchi inapokuwapo misafara ya viongozi. Miaka yote ilikuwa kuna mabango ya kudai hospitali hazina dawa, ila mwezi uliopita amekwenda Mhe. Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, amekwenda Mhe. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika mabango yote waliyoshika wananchi hakuna lililogusia upungufu wa dawa.
“Mabango yalikuwa yanaeleza wanavyodhulumiwa ardhi, upungufu wa maji na tumefuatilia kwa karibu kuanzia Mwanza hadi Simiyu hatukuona bango hata moja linalodai dawa. Hiyo ni ishara kuwa kuna mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa dawa nchini kwa sasa,” amesema Bwanakunu.
Amesema siku za nyuma ilikuwa kila miezi mitatu wanapeleka lori moja la dawa kwa kila wilaya mbili, lakini kwa sasa dawa zinapelekwa zaidi ya lori mbili kwa kila wilaya moja. “ARVs, dawa za malaria na antibiotics ni historia. Zipo za kutosha sasa hivi kila mkoa na kila wilaya,” amesema.
Bwanakunu ametoa changamoto kwa zahanati, vituo vya afya na hospitali zote za kila ngazi nchini kuhakikisha zinakusanya mapato yanayotokana na mauzo ya dawa. “Sehemu nyingi hawana mfumo wa kukusanya mapato wanatumia utaratibu wa zamani. Tukiweza kufikia hatua ya kila mwananchi kuwa na bima, hapo tutamaliza tatizo hili, maana hakuna atakayekuwa anakutana na hela moja kwa moja, ila kwa sasa ni changamoto.
“Unakuta unaipelekea wilaya dawa za thamani kubwa, wanauza dawa zinaisha ila hela haionekani. Na hapa kinachotakiwa ni kuwa wauze, kisha fedha zirejeshwe tuweze kununua dawa nyingine. Bahati mbaya, huwezi kuwanyima dawa ukasema watu wafe kwa sababu hawajarejesha fedha maana unakuta si wagonjwa waliozitumia vibaya.
“Nadhani wakati umefika wa kuwa na fumo wa elektroniki wa kukusanya mapato katika hospitali zote nchini kudhibiti udokozi unaoendelea kwa baadhi ya hospitali. La pili ni wizi wa dawa, viongozi wa maeneo husika wanapaswa kudhibiti watendaji wao maana kiasi cha dawa kinachopelekwa kinafahamika, hivyo hakuna sababu ya kutokuwapo nikirejea taarifa za kiwango cha dawa zilizopo. Tukifika kila wilaya tunabadika hadi ubaoni dawa zilizopokewa. Sasa tusaidiane kudhibiti wizi wa dawa huko vituoni na hospitalini,” amesema.
Kwa upande wa Kanda ya Iringa, kutokana na umbali wa kusambaza dawa mkoani Ruvuma, MSD nako wamefanya uamuzi wa kujenga Kanda ya Songea. Kwa sasa Kanda ya Iringa inahudumia mikoa mitatu ya Iringa, Njombe na Ruvuma, ambayo ina jumla ya wateja 583. Kati ya wateja hawa zipo hospitali za mikoa 3, hospitali za wilaya, hospitali teule, zahanati, taasisi za kidini (FOB) na vituo vya afya.
Umbali wa kutoka Iringa hadi Ruvuma ni kilomita zaidi ya 500. Kwa maeneo mengine kama Nyasa umbali ni kilomita hadi 700. Kutokana na changamoto hii, ni wazi kuwa MSD imekuwa haitoi huduma ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba kwa ufanisi katika mkoa wa Ruvuma siku zilizopita. Kumaliza tatizo hilo, wameamua kufungua Bohari ya Dawa Ruvuma itakayohudumia mkoa huu.
Mkoa wa Ruvuma una wananchi zaidi ya milioni 1.3, hivyo idadi hii inastahili kupata Kanda ya MSD. Hatua hii inaaminika itapunguza gharama za usambazaji, uendeshaji na kuongeza ufanisi na upatikanaji wa dawa, hali ambayo hatimaye itaiongezea MSD kipato. Mkoa wa Ruvuma kupitia kwa Katibu Tawala, tayari umewapatia MSD kiwanja cha kujenga Bohari hiyo na wanasema fedha za kuijenga zipo kama ilivyo kwa Bukoba.
Bohari hii inatarajiwa kuhudumia wilaya za Tunduru, Nantumbo, Songea (M&V), Mbinga (M&V) na Nyasa. Pia Wilaya ya Ulanga baada ya Songea kujengwa kuna kila dalili kuwa itahudumiwa na Iringa, ambako kuna umbali wa kilomita 200 ikilinganishwa na umbali wa kilomita 900 kutokea Dar es Salaam hadi Ulanga. Makete tayari iliishaanza kuhudumiwa na Kanda ya Iringa kwa nia ya kupunguza umbali kutoka kilomita 360 za kutoka Mbeya hadi 90 za kwenda Iringa.
Kwa sasa MSD inazo Kanda 8 zenye Bohari kamili ambazo ni Kanda ya Tabora inayohudumia mikoa ya Kigoma na Tabora. Kanda ya Mwanza inayohudumia mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Kanda ya Mbeya mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa, Kanda ya Iringa – mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma.
Kanda nyingine ni Mtwara – mikoa ya Mtwara na Lindi, na wilaya moja ya Mkoa wa Ruvuma. Kanda ya Moshi – mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Kanda ya Dodoma – mikoa ya Singida na Dodoma. Kanda ya Dar es salaam – mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Pwani.
Pia kuna Kituo cha Mauzo cha Tanga kinachohudumia mkoa wa Tanga na baadhi ya wilaya za Manyara na Kilimanjaro. Kituo cha Mauzo cha Muleba kwa sasa kinahuduma mkoa wa Kagera na wilaya mbili za Geita.
Wiki ijayo tutakuletea sehemu ya tatu ya mfulululizo wa makala hizi inayoonyesha mpango wa MSD kuingia ubia na wawekezaji kwa nia ya kujenga viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba nchini. Usiikose nakala yako.
8614 Total Views 10 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!