Padre Dk Faustin Kamugisha
Kujiamini ni sababu ya mafanikio. “Kujiamini! Kujiamini! Kujiamini! Huo ni mtaji wako,” alisema John Wanamaker. Kujiamini ni raslimali yako. Safari kuelekea kwenye jiji la mafanikio inahitaji mafuta yanayoitwa kujiamini.
Uwezekano wa kushinda unazidi hofu ya kushindwa. Jiaminishe na hilo. Kama hujavaa vazi la kujiamini hujavaa vizuri. Unapopoteza kujiamini, umepoteza kila kitu. Unapojiamini unaweza kupata kila kitu.
Ukweli huu Boiste aliuweka katika maneno mengine: “Yeye ambaye amepoteza kujiamini hawezi kupoteza kitu kingine zaidi.” Kujiamini ni kuwa na imani kuwa una uwezo wa kufanya jambo. Mwanafunzi asiyejiamini anaweza kuandika jibu sahihi wakati wa kufanya mtihani baada ya muda akalifuta.
Rais mstaafu wa Marekani Baraka Obama alikuwa na kauli mbiu wakati wa kampeini: “Ndiyo, tunaweza.” Alikuwa na imani kuwa wana uwezo wa kufanya jambo na uwezo wa kushinda. “Wewe ni mtu pekee duniani anayeweza kutumia uwezo wako,” alisema Zig Ziglar.
Usijidharau. Una kipaji fulani, una uwezo fulani, una utaalamu fulani, una kitu kinachokufanya kuwa wewe ambacho wengine hawana.  
“Utaalamu na kujiamini ni jeshi ambalo halishindwi,” alisema George Herbert. Hayo mawili ni mambo makubwa kiasi kwamba yanaitwa jeshi. “Kujiamini ni hisia ambapo akili inajiingiza katika jambo kubwa na la kuheshimika ikiwa na tumaini la uhakika na imani kwa yenyewe,” alisema mwanafalsafa wa Kigiriki Cicero.
Unapouza uza kwa kujiamini. Unaponunua nunua kwa kujiamini. Unapoongea na mteja ongea kwa kujiamini. Unapojinadi, jinadi kwa kujiamini. Unapojibu maswali wakati wa kusahiliwa jibu kwa kujiamini. Unapochangia hoja baada ya utafiti, changia kwa kujiamini. “Kukosekana kwa kujiamini si matokeo ya mambo kuwa magumu; ugumu unatokana na kukosa kujiamini,” alisema mwanafalsafa wa Kigiriki Seneca.
Namna gani unaweza kujiamini? Kwanza ni maandalizi. “Kujiamini ni maandalizi. Mambo mengine yapo nje ya uwezo wako,” alisema Richard Kline. Kama umejiandaa vizuri utajiamini. Pili ni kujipa thamani kubwa. Ukijipa thamani ndogo, uwe na uhakika dunia haitapandisha thamani yako. Wewe ni wa thamani.
Tatu,  ni utayari wa kupokea maswali. “Kujiamini ni kama sanaa, hakutokani kamwe na kuwa na majibu yote; bali kunatokana na kuwa tayari kupokea maswali,” alisema Earl Garly. Ukileelewa swali juu ya tatizo ambalo halina budi kutatuliwa ni kama swali linakuwa limejibiwa nusu.
Nne, kufikiria kuwa unaweza. “Kama unafikiria unaweza au huwezi, uko sahihi,” alisema Henry Ford.
Tano, jifunze kuwa rafiki wa nafsi yako mzuri sana. “Lazima tujifunze kuwa rafiki wa nafsi zetu wazuri sana kwa sababu tunashindwa kwa urahisi tunapoingia kwenye mtego wa kuwa maadui wabaya sana wa nafsi zetu,” alisema Roderick Thorp. Unapojidharau unakuwa adui wa nafsi yako. Adui wa mtu ni mtu mwenyewe.
Sita, ambatana na watu wanaokuinua, wanaojua uwezo wako mkubwa na kukufagilia. “Usithubutu, zaidi ya dakika moja kuzungukwa na watu ambao hawajui thamani yako kubwa,”alisema Jo Blackwell-Preston.
Saba, fikiria kufanikiwa. “Fikiria kama malkia. Malkia haogopi kushindwa. Kushidwa ni jiwe lingine la kuvukia kuendea ukuu,” alisema Oprah.  Kujiamini kunasimama katikati ya kutojiamini na kujiamini kupita kiasi.
Mtu inabidi abebe mawe mawili mfukoni. Moja liwe na maneno haya: “Kwa ajili yangu dunia iliumbwa.”  Lakini lingine liwe na maneno haya: “Mimi ni udongo na udongoni nitarudi.” Maneno ya kwanza yanasaidia kujiamini. Sentensi ya pili inasaidia kutopitiliza katika kujiamini. Ipo siku tutaiaga dunia. Fadhila inasimama katikati.
 
14091 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!