Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga

Watu 19 wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha magari manne ikiwemo treka wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Ajali hiyo imetokea katika barabara ya Isaka kwenye kijiji cha Mwakata halmashauri ya Msalala.

Ajali hiyo imetokea jana Agosti 8,mwaka huu, majira ya saa 4, usiku, ikihusisha gari ndogo aina ya IST (T880 DUE), Hiace (T350 BDX), lori (T658 DUW) na trekta.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali,inadaiwa kuwa trekta hilo lilikuwa likiendeshwa bila kuwa na taa za tahadhari (hazard) na kusababisha kugongana na uso kwa uso na Hiace.

Afisa muuguzi wa hospitali ya Manispaa ya Kahama, Wilbert Mollel amesema kuwa jumla ya maiti 19 zimepokelewa sambamba na majeruhi 15.

Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoani Geita ACP. Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa dereva wa trekta ambaye ni chanzo cha ajali amekimbia na juhudi za kumsaka zinaendlea.

Aidha Uongozi wa Mkoa wa Shinyanga ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Sophia Mjema umefika eneo la tukio na kulitaka jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kusimamia sheria ili kuepukana na vifo vinavyoepukika.

By Jamhuri