Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Vyuo, kuwekeza katika tafiti hususan za sayansi na teknolojia ili kuinua viwango vya tafiti na ubora wa elimu nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri, uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Amesema Kupitia Mpango huo, sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya elimu kwa kufadhili tafiti na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la ajira.

Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Taasisi za elimu na Sekta binafsi nchini kuzingatia maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia duniani katika utekelezaji wa Mpango huo.  Amesema Vyuo na Sekta binafsi vishirikiane kubaini ujuzi muhimu unaohitajika sasa na siku zijazo hususan katika fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu ili kuwezesha vijana kushindana na kupata nafasi katika soko la ajira  nchini na kimataifa.

Makamu wa Rais amesema ushirikiano baina ya Taasisi za elimu na Viwanda ni hitaji la lazima katika dunia ya leo, kwa kuwa  Vyuo haviwezi tena kuwa visiwa vya nadharia, na viwanda haviwezi kukua bila nguvukazi yenye ujuzi unaoendana na teknolojia na ushindani wa soko.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam kwaajili ya Uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda, leo tarehe 09 Februari 2026

Ameongeza kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele cha kimkakati katika kukuza ujuzi, stadi, maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri miongoni mwa vijana na wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu, ikitambua kwamba maendeleo endelevu ya Taifa hayawezekani bila kuwa na rasilimaliwatu iliyoelimika na yenye uwezo wa kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa ya sera na mitaala ya elimu katika ngazi zote kwa lengo la kuujenga mfumo wa elimu ulio mnyumbufu, jumuishi na unaoendana na vipaji, mwelekeo na mahitaji halisi ya soko la ajira, huku ikizingatia mabadiliko ya teknolojia na ushindani wa kitaifa na kimataifa.

Uzinduzi wa Mpango huo ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo aliahidi kuanzisha Mpango wa pamoja kati ya Waajiri, Vyuo vya ufundi stadi na Vyuo Vikuu kwa lengo la kulinganisha mafunzo na mahitaji halisi ya sekta za kipaumbele za Taifa, ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kwake.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa na Viongozi mbalimbali wakati akishiriki Uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.

Pamoja na mambo mengine, Mpango wa ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda unalenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya utoaji wa elimu na utendaji kazi, kwa lengo la kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele kama nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na viwanda vya kuongeza thamani. Aidha, Mpango unaweka msingi thabiti wa kujenga kizazi cha wahitimu wenye uwezo wa kuajirika, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwani umedhamiria kubadilisha mfumo wa elimu ya nadharia kwenda mfumo unaozingatia ujuzi, vitendo, ubunifu na uzalishaji mali.

Uzinduzi huo, umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge, Dini pamoja na wadau wa maendeleo. Wengine waliohudhuria ni pamoja na Waajiri na Wamiliki wa Viwanda, Wakuu wa Taasisi mbalimbali, Wakuu wa Vyuo pamoja na Wanafunzi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (kulia) pamoja na Viongozi mbalimbali, wakionesha Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda mara baada ya kuuzindua katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, akiwa na Viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na baadhi ya Waajiri, mara baada ya kuzindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 09 Februari 2026.