……………………………………………..

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wanawake wanaoshiriki mafunzo ya Female Future Program msimu wa 11, yanayotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wamechangia shilingi milioni 30 kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Fedha hizo zitagharamia upasuaji wa moyo kwa watoto saba wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi ambazo hazina uwezo wa kulipia matibabu, na kurejesha tumaini la maisha bora kwa watoto hao.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea mchango huo iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alithamini mchango wa wanawake wa Female Future Program na kuulinganisha na mchango wa wanawake wa JKCI waliopo mstari wa mbele katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo na kuokoa maisha yao.

“Mmefanya jambo la kipekee kufika hapa JKCI kuona jinsi wanawake wenzenu wanavyotoa mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya wagonjwa na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zinazowanufaisha wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema JKCI inaikomboa Afrika katika masuala ya moyo kwani ni Taasisi pekee inayofanya kambi maalumu nyingi za uchunguzi na matibabu ya moyo ambazo zimekuwa zikiwaibua wagonjwa wa moyo katika bara la Africa.

“Bado uhitaji ni mkubwa ni lazima sisi tujiongeze kuhakikisha tunaisaidia serikali yetu ili kila mtoto anayezaliwa na changamoto za magonjwa ya moyo asikose huduma”, alisema Dkt. Kisenge.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) ambayo imekuwa ikitafuta fedha kutoka kwa wadau mbalimbali kwaajili ya kulipia gharama za matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo wanaotibiwa JKCI, Dkt. Naizihijwa Majani alisema matibabu ya moyo ni ya gharama kubwa hivyo inabidi baadhi ya gharama ziende kwa wananchi lakini kutokana na hali ya kiuchumi ilivyo wananchi wengi wanashindwa kuzimudu gharama hizo.

“Baada ya kuanzishwa kwa HTAF stori imekuwa tofauti kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu kwani wengi wameweza kunufaika kupitia HTAF. Mwaka 2025 HTAF kupitia hafla ya chakula cha usiku iliweza kuchangisha shilingi bilioni 2.9 fedha ambazo zimesaidia upasuaji wa moyo kwa watoto 303”.

“Mchango mliotupa ni mkubwa, mmetoa kwenye mifuko yenu na kuweka katika kikapu kimoja kusaidia watoto wetu, kwa niaba ya watoto wote watakaonufaika kupitia mchango wenu tunawashukuru sana”, alisema Dkt. Naizihijwa.

Naye Mwakilishi wa wanawake washiriki wa Female Future Program, Mhandisi Ester Christopher alisema wameungana kama wanawake viongozi kuhakikisha wanarejesha tumaini kwa watoto wenye magonjwa ya moyo, wanafurahi kuona mchango wao wa shilingi milioni 30 utasaidia upasuaji wa watoto saba.

Mhandisi Ester alisema wanawake hao ambao ni viongozi kutoka katika Taasisi mbalimblai walipambana na kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanachangia kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.

“Tunaupongeza uongozi wa HTAF kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwa daraja la kuhakikisha watoto wanapata matibabu lakini pia tunaupongeza uongozi wa JKCI na wataalamu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuokoa maisha na kurejesha tumaini kwa wagonjwa wa moyo”, alisema Mhandisi Ester.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba-Doran alisema viongozi hao hawajamuangusha kwani wametekeleza kwa vitendo somo la uwajibikaji walilojifunza wakati wa mafunzo yao.

“Katika kurudisha kwa jamii viongozi wanawake ambao ni washiriki wa mafunzo ya Female Future Program msimu 11 wameweza kufika hapa na kutoa mchango wao, tunaomba kwa unyenyekevu mkubwa mpokee mchango wetu ambao tunaamini utaweza kusaidia na kuokoa maisha”, alisema Suzanne