Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, ametoa wito kwa shule zote za msingi na sekondari mkoani Pwani ambazo bado hazijaanzisha klabu za kupinga rushwa, kuhakikisha zinaanzisha klabu hizo huku taasisi hiyo ikiwa tayari kuzifikia na kutoa elimu.

Wito huo umetolewa Machi 12, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU wilayani Mafia lililojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 397.6.

Chalamila amesema vijana wana wajibu mkubwa katika kuzuia na kuelimisha jamii dhidi ya vitendo vya utoaji na upokeaji wa rushwa ili kujenga taifa la wananchi wenye maadili mema na uzalendo.

Alisema TAKUKURU inaamini kuwa kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha vijana kuichukia rushwa, taifa litajenga kizazi cha wazalendo wasioivumilia .

Aidha, ametoa rai kwa viongozi wa dini, vyama vya siasa, vyama vya kijamii na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kuvikataa vitendo vya rushwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Mafia, Juma Swalehe, amewasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kufichua vitendo vya rushwa, akiahidi kuwa uwepo wa jengo hilo jipya utawapa hamasa ya kuongeza uwajibikaji katika kuzuia mianya ya rushwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga fedha za ujenzi wa jengo hilo pamoja na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo wilayani humo ikiwemo ya maji na umeme inayowanufaisha wananchi.