‎Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imedhamiria kujenga barabara zote zinazounganisha mkoa wa Katavi kwa lami ili kuufanya mkoa wa kimkakati na kibiashara.

‎Amesema hayo koani Katavi alipoweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Kagwira-Ikola- Karema yenye urefu wa km 112.

‎Dkt. Nchema amesema barabara hiyo inaunganisha mji wa Mpanda na ziwa Tanganyika kwenye bandari ya Karema itachochea huduma za bandari na shughuli za kiuchumi itakapokamilika.

‎” Tumedhamiria kuunganisha barabara zenu za Rukwa- Mpanda na Mpanda -Kigoma kwa lami ili kuifanya Katavi mkoa wa kimkakati na kiuchumi”, amesisitiza Dkt. Nchemba.

‎Nae Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema Serikali imeipandisha hadhi barabara ya Kagwira- Karema kutoka kuwa barabara ya mkoa kuwa barabara Kuu hivyo ujenzi wake utakuwa wa viwango vya juu ili kuwezesha magari makubwa kupeleka na kuchukua mizigo katika bandari ya Karema ambayo ujenzi wake umekamilika.

‎” Katika kuhakikisha ujenzi wa barabara hii unakamilika kwa wakati na ubora tumeugawa sehemu mbili ambazo ni Kagwira-Kasekese km 54.1 na Kasekese- Karema km 56″, amesema Eng. Kasekenya.

‎Barabara hiyo yenye madaraja makubwa 7 na madogo 88 inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 219 itakapokamilika.

‎Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali inaendelea kuzijenga kwa kiwango cha lami barabara za Kibaoni-Sitalike km 72 na Vikonge- Mishamo hadi Uvinza km 156 ili kuunganisha mkoa wa Rukwa, Katavi na Kigoma kwa lami na hivyo kuufungua ushoroba wote wa mwambao wa ziwa Tanganyika na hivyo kuchochea uchumi wa mikoa hiyo.