Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya watu wanaozua taharuki na kutoa taarifa za uzushi zinazosababisha vitendo vya uvunjifu wa amani kuhusiana na kuibiwa kwa nyeti zao mara baada ya kushikwa bega kuacha mara moja.
Aidha linakemea na kutoa onyo kali kwa wale wanao andaa maudhui ya uongo na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii kuacha kwani hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amesema kuwa
lilifanya misako dhidi ya watu hao na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 85 kwa tuhuma hizo, kati ya watuhumiwa 16 wameshafikishwa mahakamani, watuhumiwa 69 taratibu za kisheria zinakamilishwa ili waweze kufikishwa mahakamani.
Amesema Aprili 9,2026 watuhumiwa watatu ambao ni Onia Bahati Sanga (20) mkazi wa Ntokela na Regan Joshua Kaseke (20) mkazi wa Uyole walifikishwa Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Rungwe. Watuhumiwa walitenda kosa hilo kati ya Aprili 5 na 6, 2026 huko Ntokela, Wilaya ya Rungwe.
Mtuhumiwa Hashimu William Mwanasenga (29) mkazi wa Mahango alifikishwa Mahakama ya Mwanzo Ilongo Wilaya ya Mbarali baada ya Kutenda kosa hilo Aprili 7, 2026 katika Kijiji cha Mahango Wilaya ya Mbarali.
Watuhumiwa wote watatu walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na kuzua taharuki kwa kueleza kuibiwa nyeti zao baada ya kushikwa bega.

