Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salaam

Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu (HESLB) ambao tayari wamehitimu vyuo vikuu wameshauriwa kuanza kurejesha mikopo yao kidogo kidogo ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wengine wenye uhitaji kupata fursa ya kusoma.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Wanu Hafidh Ameir wakati wa uzinduzi wa kampeni iliyoanzishwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ijulikanayo kama “Kiduchu Fresh Tunasonga”, inayowahamasisha wanufaika kuanza kurejesha kuanzia kiasi cha shilingi 5,000.

Amesema Serikali inaendelea kuthamini na kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuongeza bajeti ya mikopo kila mwaka, licha ya gharama za elimu ya juu kuendelea kuongezeka.

“Tunatambua kuwa Serikali inajali sana elimu, ndiyo maana imekuwa ikiongeza fedha kila mwaka ili kusaidia wanafunzi wengi zaidi. Hata hivyo, siyo wote wenye uwezo, hivyo wale walionufaika wanapaswa kujitathmini na kurejesha kidogo kidogo ili kusaidia wengine,” amesema Amiri.

Aidha, amezishauri taasisi binafsi zilizoajiri wahitimu waliowahi kunufaika na mikopo hiyo kushirikiana na Bodi ya Mikopo kwa kuwasaidia kukata marejesho ya mikopo moja kwa moja kutoka kwenye mishahara yao.

Ameir amesisitiza kuwa kampeni ya Kiduchu inalenga kuhamasisha utamaduni wa ulipaji wa hiari, hata kwa kiasi kidogo, ili kupunguza mzigo wa madeni kwa wanufaika.

“Kiduchu ni kidogo kidogo; hata kiasi kidogo kinaweza kusaidia kurejesha mkopo na kutoa nafasi kwa wengine,kunufaika ” amesema Wanu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo(HESLB), Dk. Bill Kiwia, amesema jumla ya shilingi trilioni tisa zimetolewa kama mikopo kwa wanafunzi, huku sehemu kubwa ikiwa bado haijarejeshwa.

Amesema mikopo yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 2.7 tayari imeiva na inapaswa kurejeshwa na wanufaika zaidi ya laki tisa.

Dk. Kiwia ameongeza kuwa kampeni ya Kiduchu inalenga kuwafikia wanufaika wengi zaidi, hususan wale walioko katika sekta isiyo rasmi, ili kuongeza makusanyo na kuboresha uendelevu wa mfuko.

Amebainisha kuwa kampeni hiyo pia inalenga kujenga historia nzuri ya mikopo kwa wanufaika, jambo litakalowasaidia kupata huduma za kifedha katika taasisi mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wDkt. Bill Kiwia, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali Katika Miaka hivi Karibuni Serikali imetoa Zaidi ya Shilingi Trilion4.6 kuwezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kupata mikopo.

Naye mchekeshaji maarufu, Teacher Paul, amesema kuwa awali ilikuwa changamoto kwa baadhi ya wanufaika kurejesha kiasi kikubwa cha fedha mara moja, lakini kupitia kampeni hiyo, hata wanaojiajiri au wasiokuwa na ajira rasmi wanaweza kurejesha kwa urahisi.

Amesema kiasi cha shilingi 5,000 ni kidogo na kinaweza kulipika na mtu yeyote, hivyo kusaidia kuhakikisha mfumo wa mikopo unaendelea kunufaisha vizazi vijavyo.