Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi
Kampuni ya Equinor kutoka Norway, ambayo ni miongoni mwa makampuni yanayotarajiwa kuwekeza katika mradi wa gesi asilia (LNG), imefanya ziara katika Bandari ya Mtwara kujionea maboresho yanayoendelea kufanyika katika bandari hiyo kwa ajil ya utayari wa utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ukiwa na thamani inayokadiriwa kuzidi shilingi trilioni 100, na unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya uwekezaji katika sekta ya nishati nchini.
Katika ziara hiyo, mwakilishi wa Equinor, Bw. Noel Cox, aliambatana na mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Bw. Asiad Mrutu, ambapo walipata fursa ya kujionea hali halisi ya utayari wa bandari hiyo kupokea na kuhudumia mizigo mikubwa ya mradi huo.
Akiwasilisha taarifa kwa ujumbe huo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Mtunze Sudi, alisema maboresho makubwa yaliyotekelezwa bandarini hapo yameongeza kwa kiasi kikubwa uwezo na ufanisi wa bandari kuhudumia shehena kubwa za mizigo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika kuboresha miundombinu ya bandari hii, hatua inayowezesha kuhudumia mizigo mikubwa kwa ufanisi zaidi,” alisema Bw. Sudi.
Aliongeza kuwa maboresho hayo yanaakisi utayari wa bandari hiyo katika kuhudumia aina mbalimbali za mizigo na kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa.
Miongoni mwa maboresho yaliyotekelezwa ni pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu ya kupakia na kushusha mizigo, kuongezeka kwa ufanisi wa utoaji huduma, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa shughuli za bandari.
Kwa mujibu wa Bw. Sudi, hatua hizo zimeifanya Bandari ya Mtwara kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya miradi mikubwa ya kimataifa, ikiwemo mradi wa LNG.
“Hali hii imeongeza utayari wa bandari yetu kuhudumia shughuli za mradi mara utakapoanza,” alisisitiza.
Aidha, aliwahakikishia wageni hao kuwa bandari ipo tayari kutoa huduma wakati wowote zitakapohitajika, huku uongozi wake ukiwa umejipanga kuhakikisha utoaji wa huduma bora, za haraka na zenye viwango vya kimataifa ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Ziara hiyo inaonekana kuwa hatua muhimu katika maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa LNG, unaotarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda na kuimarika kwa sekta ya nishati nchini.
Tanzania imegundulika kuwa na akiba kubwa ya gesi asilia katika ukanda wa pwani wa Lindi na Mtwara, rasilimali inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa viwanda mbalimbali, hususan uzalishaji wa bidhaa kama saruji na chuma.
Miongoni mwa manufaa ya mradi huo ni pamoja na kuongezeka kwa ajira kupitia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kukuza viwanda vya ndani, pamoja na kuongeza mapato ya taifa kwa manufaa ya Watanzania.



