Na Mwandii Wetu

​Baada ya kipindi kirefu cha mvutano, vilio, na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wamiliki wa vyombo vya usafiri nchini, Serikali hatimaye imetoa majibu ya kisheria kufuatia kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Kupitia Gazeti la Serikali toleo la Aprili 17, 2026, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza rasmi viwango vipya vya nauli kwa mabasi ya masafa marefu, daladala, pamoja na usafiri wa teksi na pikipiki za mtandao.

​Hatua hii imekuja ikiwa ni utekelezaji wa mamlaka ya LATRA chini ya kifungu cha 19 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini, Sura ya 413, inayopewa jukumu la kupanga na kufanya mapitio ya tozo za huduma za usafiri.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA, Prof.Ahmed M. Ame, nauli hizi mpya zitaanza kutumika rasmi ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kutangazwa kwake.

​Mchanganuo wa nauli mpya

​Katika mabadiliko hayo, mabasi ya masafa marefu (mikoani) yamegawanywa kulingana na daraja la basi na hali ya barabara. Kwa basi la daraja la kawaida (Ordinary) linalopita kwenye lami, nauli itakuwa Shilingi 57.93 kwa kila kilomita moja, huku yale yanayopita barabara za vumbi yakitoza Shilingi 66.62.

Kwa mabasi ya daraja la kati (Semi-Luxury), nauli imepangwa kuwa Shilingi 74.18 kwa kilomita kwenye barabara ya lami.

Kwa kikokotoo hiki, maana yake safari ya kutoka Dar kwenda Mwanza sasa nauli inakuwa 75,746.94 kwa daraja la kawaida na 84,342.66 kwa basi la daraja la Kati badala ya nauli ya awali ya nauli za awali.

Vivyo hivyo safari ya Dar es Salaam kwenda Tunduma kwa 61,623.5 kwa daraja la kawaida na 68,616.5 kwa basi la daraja la kati.Nauli ya usafiri wa Dar es Salaam kwenda Kyela sasa itakuwa ni 60,757.62 kwa daraja la kawaida na 67,652.16 kwa daraja la kati.

​Kwa upande wa mabasi ya mijini, maarufu kama daladala, nauli zimepangwa kwa kufuata umbali:

​Kilomita 0 – 10: Shilingi 700.
​Kilomita 11 – 15: Shilingi 800.
​Kilomita 16 – 20: Shilingi 900.
​Kilomita 21 – 25: Shilingi 1,000.

​Viwango vinaendelea kupanda hadi kufikia Shilingi 1,500 kwa safari za kilomita 36 hadi 40.
​Hata hivyo, Serikali imeweka kinga kwa wanafunzi, ambapo nauli yao kwa mabasi ya mijini itaendelea kuwa Shilingi 200 kwa safari zote, bila kujali umbali wa njia.

​Teksi na Pikipiki Mtandao

​Kwa mara ya kwanza, LATRA imeweka bayana viwango vya usafiri wa kidijitali. Kwa teksi mtandao zenye uwezo wa kubeba abiria wanne, nauli ya kuanzia safari (tripu) itakuwa kati ya Shilingi 1,100 na 1,200, huku nauli kwa kila kilomita ikiwa ni kati ya Shilingi 1,100 na 1,300.

Kwa upande wa pikipiki (Bodaboda mtandao), nauli ya kuanzia imewekwa kuwa kati ya Shilingi 400 na 500, na nauli ya kilomita ikiwa katika kiwango hichohicho.
​Kauli za Viongozi na Wadau
​Uamuzi huu umepokelewa kwa hisia tofauti, lakini wamiliki wengi wa vyombo vya usafiri wameuona kama mkombozi.

Mmoja wa viongozi wa vyama vya wasafiri amekaririwa akisema kuwa ongezeko hili litasaidia kupunguza makali ya bei ya mafuta na vipuri ambayo yamekuwa yakipanda kila kukicha.

​”Tumekuwa tukipiga kelele kwa muda mrefu kuhusu gharama za uendeshaji. Ingawa hatujapata kila tulichotaka, hatua hii ya LATRA ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha biashara ya usafirishaji haifi,” alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake mara moja.

​Naye Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA amesisitiza kuwa mamlaka itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa viwango hivi ili kumlinda mlaji. Amesema mtoa huduma yeyote hatozwi nauli inayozidi kiwango kilichowekwa, na ni lazima aweke wazi viwango hivyo kwa abiria. Aidha, ni marufuku kumtoza abiria tozo yoyote ambayo haijaidhinishwa na Serikali.

​Hatua za Baadaye
​Mabadiliko haya yanakuja wakati ambapo wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama za maisha. Hata hivyo, wachumi wanasema kuwa bila kufanya mapitio haya, sekta ya usafirishaji ingekuwa hatarini kusimama, jambo ambalo lingekuwa na athari kubwa zaidi kwa uchumi wa taifa.

​LATRA imetoa onyo kali kwa wamiliki watakaokiuka taratibu hizi na kuanza kutoza nauli kabla ya muda wa siku 14 uliowekwa kisheria kukamilika. Kila mdau wa usafiri anahimizwa kuzingatia umbali, muda, na aina ya huduma kama ilivyoainishwa kwenye jedwali jipya la nauli ili kuepuka faini na hatua za kisheria.