Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kukua kwa kasi nchini, huku takwimu zikionesha ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma mbalimbali za kidijitali
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Aprili 30, 2026
Wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo, ambapo amesema kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 90.4 Machi 2025 hadi milioni 111.9 Machi 2026, sawa na ongezeko la asilimia 23.8, hali inayoashiria kuongezeka kwa upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano nchini.
Amesema pia watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 49.3 hadi milioni 58.9 katika kipindi hicho, ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.5, wakati watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu (mobile money) wameongezeka kutoka milioni 66.5 hadi milioni 81.0, sawa na asilimia 21.8.
Kwa upande wa watoa huduma, Kairuki amesema idadi ya watoa huduma wa miundombinu ya mawasiliano imeongezeka hadi 52 Machi 2026 kutoka 38 Machi 2025, sawa na ongezeko la asilimia 36.8, huku watoa huduma za ziada (Application Services and Value-Added Services) wakifikia 173 kutoka 136, ongezeko la asilimia 27.2.
Waziri Kairuki amesema ukuaji huo umetokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na ujenzi wa minara ya mawasiliano, ambapo Kata 688 nchini zimefikishiwa huduma hizo na kunufaisha wananchi takribani milioni 8.5.
Aidha, amesema uunganishaji wa Mkongo wa Taifa katika wilaya 86 umeimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa njia ya kidijitali, pamoja na kuimarisha mfumo wa Anwani za Makazi unaosaidia utambuzi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Kairuki amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa dira ya Serikali katika kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi nchini.


