Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amesema kuwa Serikali imeanza kutekeleza kikamilifu ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuwawezesha vijana katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), hususan katika kuendeleza kampuni changa za kidijitali.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Alhamisi Aprili 30, 2026, Waziri Kairuki amesema kuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025, Rais Samia aliahidi kutenga Shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya kuwezesha biashara ndogo, za kati na kampuni changa, ambapo Shilingi Bilioni 5 kati ya hizo zimetengwa mahsusi kwa kampuni changa za TEHAMA.

“Fedha hizo tayari zimepatikana na maandalizi ya mwongozo wa upatikanaji wa mikopo yamekamilika. Utoaji wa mikopo utafanywa kupitia Benki ya NMB, na unatarajiwa kuanza mwezi Mei 2026 kwa kampuni zitakazokidhi vigezo.” alisema Kairuki

Waziri Kairuki ameongeza kwa kusema kuwa, mpango huo unalenga kuziwezesha kampuni changa zisizopungua 50 zinazojihusisha na maeneo mbalimbali ya teknolojia ikiwemo bunifu za kifedha (FinTech), Legal Tech, Entertainment Tech, Agri-Tech, Tourism Tech, Insur-Tech, Edu-Tech, Logistics-Tech, mifumo ya huduma (SaaS), e-commerce na maeneo mengine ya ubunifu wa kidijitali.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa ahadi hii ni uthibitisho wa dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali, sambamba na kukuza ajira, ubunifu na ushindani wa kimataifa.

Waziri Kairuki amehitimisha kwa kusema kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha mazingira wezeshi ya TEHAMA, kuongeza ubunifu na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha teknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.