Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amesema kuwa Tanzania imekamilisha taratibu zote za ununuzi wa vifaa vya uundaji wa satelaiti ndogo aina ya CUBESAT kupitia mradi wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Anga za Juu (UNOOSA) unaojulikana kama KIBOCUBE.

Amesema hayo leo Alhamisi Aprili 30, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Akifafanua zaidi Waziri Kairuki amesema, usajili wa satelaiti hiyo tayari umefanyika katika chombo cha kimataifa kinachoratibu shughuli za anga za juu – ITU, hatua inayoiweka Tanzania katika ramani ya mataifa yanayojiandaa kutumia teknolojia ya satelaiti kwa ajili ya mawasiliano, utafiti, usimamizi wa rasilimali na usalama.

Kukamilika kwa hatua hii kutaiwezesha Tanzania kuanza maandalizi ya mwisho ya uundaji wa satelaiti hiyo, ambayo itakuwa na matumizi mbalimbali ikiwemo kuboresha mifumo ya mawasiliano, ukusanyaji wa takwimu za mazingira, ufuatiliaji wa majanga na kuongeza uwezo wa kitaifa katika ubunifu wa teknolojia ya kisasa.

Ameongeza kwa kusema, kuwa mradi wa KIBOCUBE ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuijenga Tanzania ya kidijitali na kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani katika masuala ya anga za juu, TEHAMA na ubunifu wa kimataifa.

Hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa taifa la Tanzania katika safari yake ya kuingia rasmi kwenye teknolojia ya anga za juu na kuongeza uwezo wa kisayansi na kiufundi katika TEHAMA.