Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mashirikiano wa Shirikisho la Umoja wa Vijana wa Afrika (Pan African Youth Union) Bi. Kaoutar Moudar.

Mazungunzo hayo yamefanyika leo Aprili 30, 2026 kando ya Mkutano wa 12 wa Kikanda wa Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Aidha, mazungumzo yao yalilenga kuunganisha PYU na Kituo cha Afrika cha Vijana cha Kujenga Uwezo wa Majadiliano kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi kilichoanzishwa nchini Tanzania hivi karibuni.

PYU ni taasisi ya uratibu ya ngazi ya bara inayolenga kuunganisha vijana na kuhakikisha ushiriki wao katika michakato ya maendeleo na utungaji sera barani Afrika. 

Taasisi hiyo ina jukumu muhimu katika kukuza ushiriki wa vijana katika mifumo ya kisera katika ngazi za kitaifa na kikanda, ili kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Dkt. Muyungi amekutana na kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa Climate Investment Fund (CIF), AfDB na wawakilishi wa nchi za Visiwa za Afrika, mkutano uliohusu Fursa ya Fedha za kujenga uhimilivu wa Mabadiliko ya tabianchi kwa nchi za visiwa.

Katika mkutano huo, Dkt. Muyungi na wadau hao wa maendele wamejadili kuhusu Mpango wa uwekezaji wa ARISE chini ya Climate Investment Funds (CIF) unaolenga kuimarisha ujumuishaji wa ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi katika sera na mipango ya maendeleo ya kitaifa kupitia mbinu zinazoongozwa na nchi husika.

Imeelezwa kuwa Mpango huo unasaidia uwekezaji unaolenga kuimarisha mifumo ya kitaasisi, kuongeza rasilimali za kifedha kutoka sekta za umma na binafsi.

Pia, mpango huo ni mojawapo ya njia za kulinda jamii zilizo hatarini, na kuimarisha ustahimilivu wa mifumo muhimu ya kiuchumi na kijamii katika sekta za kilimo, nishati, maji, usafiri, miundombinu na viwanda.

Aidha, katika mkutano huo ilibainishwa kuwa Programu ya ARISE imetangaza ufadhili wa takriban dola milioni 30 hadi 40 kwa programu za nchi zenye sifa na hadi dola milioni 50 kwa programu za kikanda.


Pamoja na mikutano hiyo, pia Dkt. Muyungi alishiriki uzinduzi wa Ripoti ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika Bara la Afrika, uliofanyika wakati wa Mkutano wa 12 wa Kikanda wa Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu.

Itakumbukwa kwamba mkutano huo uliofunguliwa Aprili 28, 2026 na kushirikisha viongozi mbalimbali na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali umehitimishwa Aprili 30, 2026.