Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame amewasili nchini kwa Ziara ya Kikazi ya siku moja yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa uwili kati ya Tanzania na Rwanda.
Mhe. Rais Kagame anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Inategemewa kwamba Ziara hii itadumisha mahusiano mazuri na ya kihistoria kati ya majirani hawa wawili. Ushirikiano huu umezidi kuimarika katika miaka ya hivi karibuni kwa kupitia Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC), ambapo Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa washirika wakuu watatu wa biashara wa Rwanda duniani, huku kiwango cha biashara kati ya nchi hizi kikiongezeka kila mwaka.
Aidha, katika uwekezaji, kuanzia mwaka 1990 hadi Machi 2026, Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.53 na kuunda ajira 2,225 katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, usafirishaji, huduma za kifedha, maliasili na utalii.
Vilevile, wawekezaji wa Tanzania pia wamewekeza nchini Rwanda kupitia kampuni mbalimbali zikiwemo Bakhresa Group, Magodoro Dodoma, Discount Center, Jambo Plastic, Sagar Enterprises, Buffalo Travelling Tours, Maxcom Africa, Gasabo Grain Milling Company, LCM Delta Company na Metrex Integrated Consultancy.











