Na Allan Ntana, JamhuriMedia, Tabora
SERIKALI Mkoani Tabora imesema kuwa omba omba walio wengi wakiwemo wale wanaosukumwa kwenye vibaiskeli wana uwezo wa kufanya kazi zinazoweza kuwaingizia kipato na sio kukaa au kujipitisha mitaani wakiomba.
Akihutubia Watumishi wa Umma na wa Sekta Binafsi kwenye Maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika Kimkoa Wilayani Kaliua Mkoani hapa jana, Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha amepiga marufuku ombaomba wanaojipitisha au kukaa mitaani.
Ameeleza kuwa serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kusaidia kaya zote zisizo na uwezo, hivyo omba omba wote wanapaswa kutambuliwa na kuingizwa katika mfuko huo na sio kuomba omba mitaani.
‘Wengi wao ni watu wazima ambao wana uwezo wa kufanya kazi na hata wale wanaowasukuma kwenye vibaiskeli hawana shida yoyote, hawa hawapaswi kuwa omba omba, wanapaswa kuwepo kwenye mfuko huo’, ameeleza.
Chacha amesisitiza kuwa serikali iliweka utaratibu wa kusaidia wale wote wasio na uwezo (kaya maskini) kupitia mfuko huo wa maendeleo ya jamii, lakini utakuta wakiendelea kuomba omba mitaani, zoezi la kuwakamata limeshaanza.
Aidha, katika maadhimisho hayo RC amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Taasisi zote kuwapa ushirikiano wa dhati watumishi walio chini yao, kusikiliza hoja zao kwa wakati na sio kuwapangia siku ‘appointment’.
‘Ofisi zote ikiwemo ya Mkuu wa Mkoa tuwape ushirikiano wa kutosha watumishi walio chini yetu, mtumishi akiwa na shida sio hadi aombe ‘appointment’, kama haupo ofisini akupigie simu ili shida yake iishe’, amesisitiza.
Akiongea katika maadhimisho hayo Katibu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoani hapa Amina Mwaluko amewakumbusha waajiri wote katika Mkoa huo kuwatendea haki watumishi kwa kupeleka michango yao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati.
Amesisitiza kuwa michango hiyo ni takwa la kisheria, hivyo inapaswa kupelekwa kwa wakati na kwa ukamilifu ili ziwasaidie punde watakapo staafu au utumishi wao utakapokoma katika taasisi zao.

