Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewaomba Viongozi wa wafanyabiashara wa lililokuwa Soko la Rehema Nchimbi kukaa pamoja na uongozi wa jiji hilo ili kujadili rasimu ya mkataba wa upangaji wa eneo la Umonga.

Hatua hiyo inayolenga kumaliza mvutano unaoendelea kuhusu namna ya kuanza rasmi shughuli za biashara katika eneo hilo.

Akizungumza leo Mei 4,2026 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Halmashauri hiyo, Denis Gondwe, amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara hao wakidai kutotendewa haki katika mchakato wa kupatiwa maeneo mbadala baada ya kufungwa kwa soko lao la awali.

Gondwe amesema baada ya kufungwa kwa Soko la Rehema Nchimbi lililokuwa na wafanyabiashara zaidi ya 300 Oktoba mwaka jana, halmashauri ilipendekeza kuwapanga katika masoko mengine, lakini wafanyabiashara walikataa mpango huo.

“Baada ya kukataa kwenda katika masoko yaliyopendekezwa, wafanyabiashara hao waliwasilisha malalamiko yao kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma wakitaka kupatiwa eneo jingine,” amesema Gondwe na kueleza,

kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya aliunda kamati maalumu iliyofanya tathmini na kutembelea maeneo mbalimbali, ambapo hatimaye ilipendekeza wafanyabiashara hao wapatiwe eneo lililopo Mtaa wa Kitenge lenye ukubwa wa mita za mraba 8,621,”amefafanua.

Gondwe amesema mapendekezo hayo yameridhiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuanza kwa maandalizi ya uendelezaji wa eneo hilo.

Aidha, amesema Waziri Mkuu Mwigulu Lameck Nchemba alipotembelea eneo la Umonga, aliagiza kasi ya utekelezaji iongezwe na kuhakikisha wafanyabiashara wanapatiwa mikataba iliyo wazi kabla ya kuanza shughuli zao.

Kufuatia maelekezo hayo, Gondwe amesema halmashauri iliwaita viongozi wa wafanyabiashara kupitia barua ya Aprili 24, 2026 kwa ajili ya kupitia rasimu ya mkataba wa upangaji, ambapo kikao kilifanyika Aprili 27, 2026.

Alisisitiza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma haitambui ugawaji wowote uliofanyika katika eneo la Umonga, akieleza kuwa yeyote anayedai kupewa eneo hilo nje ya utaratibu rasmi ametapeliwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Jiji la Dodoma, Nsubisi Kapula, amesema serikali iko tayari kuendelea na mazungumzo na viongozi wa wafanyabiashara ili kufikia mwafaka wa pamoja.

Amesema endapo makubaliano hayatapatikana, serikali itaingilia kati na kuhakikisha pande zote zinakutana ili kusaini mikataba rasmi ya uendeshaji wa biashara.