Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kuunga mkono kwa dhati ripoti ya Tume ya Uchunguzi kuhusu matukio ya vurugu yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku kikiahidi kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyotolewa.

Akizungumza jijini Dodoma leo Mei 4, 2026, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesema tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilifanya kazi yake kwa uhuru mkubwa na kwa kuzingatia weledi, na kwamba ripoti yake imelenga kuimarisha mshikamano na kuleta uponyaji wa Taifa.

Ameongeza kuwa chama hicho kinawashukuru Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni, hatua aliyosema imeongeza uhalali wa ripoti hiyo.

Kihongosi amesema CCM inaunga mkono mapendekezo yote yaliyowasilishwa na tume hiyo, na kwamba tayari Rais ameyapokea na kuanza kuyafanyia kazi kwa manufaa ya nchi.

“Chama kitaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu na kuhamasisha wananchi kuunga mkono juhudi hizi zinazolenga kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa njia ya maridhiano ndiyo suluhisho sahihi katika kushughulikia changamoto zilizojitokeza, huku akisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha vurugu hizo pamoja na kuwawajibisha wahusika.

Katika hatua nyingine, amesema CCM inaunga mkono kuanzishwa kwa tume ya upelelezi itakayochunguza kwa undani matukio hayo, akieleza kuwa chama kiko tayari kushiriki katika mchakato wa maridhiano kwa mfumo shirikishi unaohusisha wadau wote wa jamii.

Kuhusu Katiba Mpya
Kihongosi amesema mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya ni sehemu ya ajenda ya chama hicho na umejumuishwa katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030.

Ameeleza kuwa mchakato huo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2030.

Amefafanua kuwa juhudi za kupata Katiba mpya zilianza mwaka 2011 chini ya Serikali ya Awamu ya Nne, lakini ziliishia katika rasimu ya Katiba iliyopendekezwa kufuatia baadhi ya vyama vya siasa kujitoa katika mchakato huo.

Amesisitiza kuwa Katiba mpya ni suala la kitaifa linalohitaji ushiriki wa makundi yote ya kijamii, ikiwemo wananchi wasiokuwa na vyama vya siasa.

Vilevile, ametoa wito kwa vijana, hususan wasomi, kujiepusha na vitendo vya vurugu na badala yake kushiriki kulinda amani ya nchi, akieleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa utulivu.

Kuhusu kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, John Heche, aliyedai kuwa CCM inaazima viongozi kutoka vyama vingine, Kihongosi amesema Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umeendelea kuzalisha viongozi wengi wanaoshika nafasi mbalimbali za kitaifa.

Amedai kuwa idadi kubwa ya wakuu wa mikoa wanatokana na umoja huo, jambo alilosema linaonesha uimara wa chama katika kukuza uongozi.

Akizungumzia uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ambaye aliwahi kuhusishwa na Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Kihongosi amewataka viongozi wa Chadema kujitathmini kama Katambi alikuwa mwanachama halali wa chama hicho.