Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia Pwani
MWENYEKITI wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, ametoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuharakisha ujenzi wa barabara ya Picha Ndege–Boko Timiza (km 0.52) kwa kiwango cha lami pamoja na kuendelea kuiombea fedha ili kukamilisha mradi huo utakaorahisisha usafiri kuelekea kituo cha Reli ya Kisasa (SGR).
Mlao alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Kibaha, akisisitiza kuwa barabara hiyo ni muhimu kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa eneo hilo.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto za usafiri na kurahisisha safari za wananchi kuelekea SGR, badala ya kutumia muda mrefu kupitia Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Kamisaa wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge, alisema barabara hiyo inaunganisha mtandao muhimu wa Bokomnemela–Soga na Kongowe–Soga, akibainisha kuwa ni sehemu muhimu ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Kunenge alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara nchini, akisema uwekezaji huo unaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi mkoani Pwani.
Naye Meneja wa TARURA Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Samwel Ndoveni, alisema kutokana na changamoto za upatikanaji wa barabara hiyo wakati wa masika, serikali ilitenga fedha kwa awamu tatu kwa ajili ya ujenzi wa lami ngumu.
Alieleza kuwa hadi sasa kilomita 1.77 zimekamilika, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 shilingi milioni 760 zilitengwa kwa ujenzi wa kipande cha mita 520.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo ilikagua mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Manispaa ya Kibaha, ambapo Mhandisi wa Manispaa hiyo, John Alexander, alisema mradi huo umepokea zaidi ya shilingi bilioni 4.193 kwa awamu mbili za utekelezaji kupitia wakandarasi SUMAJKT Construction Co Ltd na Sibstone Construction Co Ltd.






