Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha kwanza imetatua na kupatia ufumbuzi jumla ya hoja 15 kati ya hoja 18 za Muungano na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano zilizokuwepo.
Hatua hiyo imeonesha dhamira ya dhati katika kuuenzi, kuulinda na kuuimarisha Muungano kwa misingi ya haki, usawa, mashauriano na maslahi ya pamoja.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Mei 12, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwera Mhe. Suleiman Mohamed Rashid aliyetaka kujua kero ngapi za Muungano zimetatuliwa katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Mhe. Kwagilwa alieleza kuwa kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumeleta ufanisi mkubwa katika utatuzi wa hoja za Muungano.

Alifafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia Hoja za Muungano kupitia Kamati hiyo mwaka 2006, jumla ya hoja 25 zimejadiliwa na hadi kufikia mwaka 2026, hoja 23 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa rasmi katika orodha ya Hoja za Muungano, huku hoja mbili zikiendelea kufanyiwa kazi.

Akijibu maswali ya nyongeza kuhusu zipi faida za utatuzi wa hoja za Muungano, Mhe. Kwagilwa alizitaja kuwa ni kufanikisha ushiriki wa Zanzibar kwenye masuala ya kimataifa na kikanda hususani katika kuandaa hoja na msimamo wa pamoja kama nchi kwenye makubaliano ya kimataifa ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki.

Sanjari na hilo, alisema pia umewekwa utaratibu mzuri wa shughuli za Uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu kupitia miongozo ambayo inaepusha migongano isiyo ya lazima katika shughuli hizo za kiuchumi.

Mhe. Kwagilwa alitaja faida nyingine kuwa ni kuondolewa mzigo wa kulipa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara kutoka Zanzibar yaani Kodi ya Mapato (PAYE) na kodi ya zuio (withholding tax) ambazo zilikuwa ni miongoni mwa malalamiko ya muda mrefu.

Itakumbukwa kuwa Hoja mbili zilizobaki zinaendelea kufanyiwa kazi kupitia mashauriano ya kisekta na maelekezo ya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ. Hoja hizo ni Mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki pamoja na faida ya Benki Kuu na hoja ya Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha pamoja na suala la Usajili wa Vyombo vya Moto.

Hivyo, utatuzi wa hoja hizo umewezesha kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili za Muungano, kuondoa malalamiko ya muda mrefu, kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika Taasisi za Muungano pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.