Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeendelea kuimarisha utoaji na udhibiti wa huduma za hali ya hewa nchini kwa lengo la kuongeza usalama, ufanisi na maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo usafiri wa anga.

Hayo yameelezwa leo Mei 13, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, wakati akiwasilisha makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo.

Profesa Mbarawa amesema TMA imekamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda na Pemba kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa kwa sekta ndogo ya usafiri wa anga.

Amesema mitambo hiyo itasaidia kuongeza usahihi wa taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kwa marubani pamoja na wadau wengine wa usafiri wa anga, hatua itakayochangia kuimarisha usalama wa safari za ndege na kupunguza changamoto zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Aidha, amesema TMA inaendelea na ujenzi wa miundombinu muhimu ya hali ya hewa ikiwemo maabara ya uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa (Calibration Center) jijini Dar es Salaam, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 46.

“Ujenzi wa maabara hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha vifaa vya hali ya hewa vinakuwa na ubora na usahihi unaohitajika katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa nchini,” amesema Profesa Mbarawa.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya hali ya hewa ili kuendana na maendeleo ya teknolojia pamoja na mahitaji ya sekta mbalimbali zinazotegemea taarifa sahihi za hali ya hewa nchini.