📍Shinyanga
Kuanzishwa kwa masoko ya madini ya almasi na dhahabu mkoani Shinyanga kumechochea kwa kasi ongezeko la uzalishaji, biashara na mapato ya Serikali, huku wachimbaji na wafanyabiashara wakinufaika na kusogezewa huduma karibu nao.
Akizungumza katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Mthaminishaji wa Madini ya Almasi, Shikimayi Muyinza, amesema uzalishaji wa almasi umeongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na kuibuka kwa machimbo mapya pamoja na uwepo wa masoko rasmi ya madini yaliyorahisisha biashara na kuongeza uwazi.
Amesema awali uzalishaji ulitegemea zaidi eneo la Maganzo karibu na Mwadui, lakini tangu mwaka jana machimbo mapya ya Ng’wapangabule yameongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa wachimbaji wadogo.
Kwa mujibu wa Muyinza, mwezi Aprili 2026 pekee karati 6,177 za almasi zilinunuliwa sokoni, tofauti na hapo awali ambapo uzalishaji haukuwa ukifikia hata karati 1,000 kwa mwezi.
“Hili ni ongezeko kubwa sana. Sasa tunapata kati ya karati 3,000 hadi 6,000 kwa mwezi kutokana na vyanzo vipya vya uchimbaji na masoko ya madini,” amesema.
Ameeleza kuwa masoko ya madini yameongeza ufanisi wa huduma kwa kutoa uthaminishaji wa haraka na wa uwazi, ambapo wachimbaji husajiliwa, madini hupimwa na kupatiwa ushauri wa thamani kabla ya kuingia kwenye mauzo.
Muyinza amefafanua kuwa tofauti na dhahabu, bei ya almasi hutegemea sifa nne muhimu ambazo ni ukubwa, umbo, rangi na ubora wa ndani wa jiwe, hivyo kila almasi huwa na thamani yake ya kipekee.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Migodi na Msimamizi wa Masoko Mkoa wa Shinyanga, Gerald Kabeho, amesema mfumo wa masoko ya madini umeondoa urasimu uliokuwepo awali na kurahisisha upatikanaji wa huduma zote muhimu ndani ya muda mfupi.
Naye Mkurugenzi wa Mwabu General Trading, Samweli Sita, amesema masoko hayo yamewaondolea wafanyabiashara changamoto ya kutafuta wanunuzi kwani sasa wauzaji na wanunuzi hukutana moja kwa moja sokoni na kufanya biashara kwa uwazi.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha masoko ya madini nchini, hatua aliyosema imeongeza fursa za biashara, kuimarisha uchimbaji halali na kukuza sekta ya madini kwa wachimbaji wadogo na wakubwa.
Takwimu zinaonesha kuwa mafanikio hayo pia yameongeza makusanyo ya Serikali ambapo kuanzia Julai hadi Aprili mwaka wa fedha 2025/2026, Mkoa wa Shinyanga umekusanya shilingi bilioni 35.2, sawa na asilimia 110 ya lengo la shilingi bilioni 32, ikiashiria mchango mkubwa wa masoko ya madini katika kukuza uchumi wa taifa.






