Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pemb

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha ACT Wazalendo Tawi la Kitunda, Jimbo la Kiwani Mkoa wa Kusini Pemba, wametakiwa kuongeza juhudi za kusajili wanachama wapya ili kuimarisha msingi wa chama hicho na kuongeza nguvu ya kisiasa katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Habari na Uenezi wa Chama Cha ACT Wazalendo Mkoa wa Mkoani Pemba, Muhammed Khamis, wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa tawi hilo.

Akihutubia mkutano huo, amesema wanachama wa ACT Wazalendo wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kila siku wanafanya kazi ya kukitangaza chama pamoja na kuwashawishi wananchi, hususan vijana, kujiunga na chama hicho ili kujenga nguvu mpya ya mabadiliko.

Amesema vijana ndio injini ya maendeleo ya taifa, lakini kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa ajira, mazingira duni ya kiuchumi pamoja na kukosekana kwa fursa sawa za maendeleo.

“Ni wajibu wetu kuwafikia vijana, kuwasikiliza na kuwapa matumaini kupitia siasa safi zenye mwelekeo wa kuleta mabadiliko halisi. Vijana hawawezi kuachwa pembeni wakati wao ndio nguzo kuu ya taifa,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa kwa miaka mingi watawala wamekuwa wakitumia ahadi za ajira kama chambo cha kisiasa kwa vijana, lakini baada ya uchaguzi ahadi hizo hubaki kuwa maneno matupu yasiyo na utekelezaji.

“Tumeshuhudia makundi mengi ya vijana wakiahidiwa ajira wakati wa kampeni, wakivalishwa sare na kutumika kama nguvu ya kisiasa. Leo ni vyema kujiuliza, ni wangapi kati yao wamepata ajira hizo walizoahidiwa?” alihoji.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa Habari na Uenezi alikabidhi kadi mpya za kielektroniki kwa wanachama 45 wa tawi hilo, huku akiwataka kuzitunza kama alama ya utambulisho na uhai wa uanachama wao ndani ya chama.

Akizungumzia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana, alisema chama kinaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu mchakato huo pamoja na hatua zinazofuata kisiasa, huku akiwataka wanachama kuwa watulivu na kuendelea kuiamini chama chao.

Alimaliza kwa kusisitiza kuwa mshikamano, nidhamu na ujenzi wa chama kuanzia ngazi ya matawi ndiyo msingi wa ushindi wa kisiasa na mafanikio ya ACT Wazalendo katika siku zijazo.