Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb) amemwakilisha Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye uzinduzi wa Kongamano la Vijana wa Kitanzania chini ya Umoja wa Mataifa (Tanzania International Model United Nations -TIMUN 2026) linalofanyika Zanzibar, Leo tarehe 18 Mei 2026.

Katika Hotuba yake, Naibu Waziri Dkt. Maghembe amesisitiza umuhimu wa nafasi ya vijana katika kuleta maendeleo endelevu na mabadiliko chanya, kupitia teknolojia, diplomasia na ubunifu katika ngazi na Taifa na Ulimwenguni.

Mkutano wa TIMUN 2026, ni jukwaa muhimu la kimataifa linalolenga kukuza viongozi vijana, wanadiplomasia, wabunifu, na mawakala wa mabadiliko ambalo hufanyika kila mwaka chini ya uratibu wa Chama cha Vijana katika Umoja wa Mataifa Tanzania (Youth of United Nations Association Tanzania-YUNA).

Mhe. Maghembe ameipongeza YUNA Tanzania kwa kuwawezesha vijana na kuendeleza maadili ya Umoja wa Mataifa miongoni mwa vijana wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Tumieni mkutano huu kubadilishana mawazo, kujenga ushirikiano, na kuibua suluhisho za changamoto mbalimbali zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa ajira, usawa wa kijinsia, na maendeleo ya teknolojia” alibaibisha Mhe. Maghembe.