Na Mwandishi Wetu, Pwani

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuboresha Vituo vya Maarifa nchini, hususan vile vinavyotoa huduma kwa madereva wa malori ya masafa marefu kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Jim Yonazi mapema mwanzoni mwa wiki mara baada ya kutembelea na kukagua Vituo vya Maarifa vinavyotoa huduma za VVU na UKIMWI kwa madereva wa malori ya masafa marefu vilivyopo eneo la Kurasini katika wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam na Mdaula mkoa wa Pwani ambayo Vituo hivyo vipo chini ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Dkt. Yonazi amesema Serikali, kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), ina jukumu la kusogeza huduma muhimu za VVU na UKIMWI karibu na wananchi.

“Vituo hivi vina mchango mkubwa katika kuwafikia madereva wa masafa marefu ambao mara nyingi hukaa safarini kwa muda mrefu. Serikali itaendelea kuviboresha hususan kwenye miundombinu ya kutolea huduma na kuongeza wataalam wa afya ili viweze kutoa huduma bora Kwa madereva hao wa masafa marefu kwa kujua afya zao dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI,” amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wao, madereva wa malori ya masafa marefu wanaonufaika na huduma hizo wameeleza kuwa Vituo vya Maarifa ni msaada mkubwa kwao, kwani vinawapa fursa ya kupata elimu na huduma za VVU na UKIMWI kwa urahisi na bila gharama na kuipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kujali na kuwafikia wananchi wake.

88888888888888888888

Ujenzi wa vituo vya afya Nkasi wafikia asilimia 97

‎Na Israel Mwaisaka, Nkasi

‎Serikali imeanza utekelezaji wa miradi minne, ikiwemo ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya na shule wilayani Nkasi mkoani Rukwa yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6, itakayosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya pamoja na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

‎Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya vya Kasu, King’ombe na Chala, pamoja na ujenzi wa Shule ya Amali ya Wilaya, ambayo inagharimu kiasi cha shilingi 583,028,083.

‎Wakisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Afraha Hassan wasimamizi wa miradi hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, walisema kuwa miradi hiyo imefikia asilimia 97 ya utekelezaji wake, ikitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 15, 2026.

‎Aidha, kupitia ziara hiyo, Afisa Wanyamapori wilayani humo, Arnold Ngagashi, alibainisha kuwa serikali imetoa jumla ya shilingi 152,709,375 kama kifuta machozi kwa wananchi 131 waliokumbwa na madhara ya wanyama waharibifu, hususan tembo waliovamia mashamba yao.

‎Alisema kuwa kati ya waliolipwa, 19 ni majeruhi, 22 walipoteza maisha, na 391 walipata uharibifu wa mazao katika eneo la ekari 890.2.

‎Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu, ikihusisha Kamati ya Siasa ya chama cha mapinduzi CCM, ikiwa na lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza changamoto pamoja na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinaendelea kuimarishwa katika wilaya ya Nkasi.