RAIS wa Marekani Donald Trump alisema alisitisha shambulio lililokuwa limepangwa dhidi ya Iran ili kutoa nafasi kwa mazungumzo mapya ya kidiplomasia, huku akieleza kuwa bado kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Trump alisema viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu walimshawishi kuahirisha mashambulizi hayo yaliyokuwa yafanyike Jumanne ili kutoa muda kwa juhudi za amani kuendelea.
Trump alisema kuna nafasi nzuri sana ya Marekani na Iran kufikia makubaliano yatakayozuia Tehran kutengeneza silaha za nyuklia bila kuingia kwenye vita vikubwa zaidi.
Hata hivyo, Rais huyo ameonya kuwa Marekani ipo tayari kuanzisha mashambulizi makubwa ikiwa mazungumzo hayo yatashindikana au Iran itakataa masharti ya makubaliano mapya.
Ripoti zimeeleza kuwa Iran imetuma pendekezo jipya la amani kupitia Pakistan likijumuisha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz pamoja na hatua za kupunguza mvutano wa kijeshi katika eneo la Ghuba.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaeleza kuwa hatua ya Trump kusitisha mashambulizi inaonyesha presha kubwa kutoka kwa washirika wa Marekani Mashariki ya Kati waliokuwa wakihofia kuongezeka kwa vita na athari zake kwa uchumi wa dunia.
Mvutano huo ni mwendelezo wa vita vilivyoanza Februari mwaka huu baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran, hali iliyosababisha taharuki katika soko la mafuta, usafirishaji wa kimataifa kupitia Mlango wa Hormuz na mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran.

