Umoja wa Waendesha Bandari Kavu Tanzania (CIDAT) umebainisha kuwa uamuzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wa kupunguza ada ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (PID) kutoka asilimia 9 hadi asilimia 4.5 ya kodi ya forodha utakuwa na faida mkubwa kwa Tanzania kwa ujumla na mtu mmoja mmoja kwani utakuwa ni kichocheo cha kuzalisha maelfu ya nafasi mpya za ajira kwa vijana.
Akizungumza kuhusu maboresho ya tozo hiyo, Mwenyekiti wa umoja huo, Bw. Meleck Shange, ameeleza kuwa upanuzi wa miundombinu ya bandari utakuwa na mnyororo chanya wa kiuchumi utakaonufaisha sekta ya usafirishaji na kuongeza uhitaji wa nguvu kazi ya vijana.
“Na katika kusikiliza kilio cha walio wengi wameweza kutoka 9% mpaka 4.5% jambo mbalo kwa kweli ni la faraja sana kwa wananchi na natumaini kwamba hata sasa hivi inapoenda kutumika basi wadau wote watakuwa tayari wako radhi kuipokea”, ameeleza Shange.
Bw. Shange amefafanua kuwa tozo hiyo itatumika kujenga magati mapya (berths) katika bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, na baadaye Bagamoyo ambapo kuongezeka kwa magati kutamaanisha meli nyingi zaidi zitafunga kwa wakati mmoja, jambo litakalosababisha shehena kubwa ya mizigo kuingia nchini na kuhamishiwa kwenye Bandari Kavu. Ujazo huu wa mizigo utalazimisha kampuni za bandari kavu kuajiri watendaji wengi zaidi ambao kwa asilimia kubwa ni vijana.

