Na Kija Elias, JamhuriMedia, Dodoma

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji amesema Serikali imejipanga kukiboresha Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA), kupitia bajeti ya mwaka 2026/2027 ili kiweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya ufundishaji, utafiti na utoaji wa ushauri wa kitaalamu katika sekta ya usimamizi wa wanyamapori pamoja na programu nyingine zinazotolewa chuoni hapo.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bungeni Jijini Dodoma, Waziri Kijaji alisema Chuo cha MWEKA kimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia upatikanaji wa taarifa za kitaalamu kwa ajili ya kufundishia, kutatua migogoro kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili na shughuli za uhifadhi na utalii nchini.

Alisema moja ya tafiti zinazofanywa na chuo hicho ni utafiti kuhusu changamoto za ufanisi wa usimamizi shirikishi wa maeneo ya jumuiya za wanyamapori nchini, ambao unalenga kuboresha ushirikiano kati ya jamii na maeneo yaliyohifadhiwa.

Katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kujifunzia kwa wanafunzi, Waziri Kijaji alisema chuo hicho kinaendelea na ujenzi wa darasa moja, jiko, vyoo na mabafu katika eneo la mafunzo kwa vitendo la Arash, Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro.

Aidha, amesema Chuo cha MWEKA kimekarabati nyumba tano za watumishi, vyumba vitano vya madarasa, hosteli nne za wanafunzi pamoja na ofisi nane za watumishi huku kikifunga meza 20 na makabati 18 katika ofisi mbalimbali za watumishi.

Kwa upande wa kuboresha mafunzo kwa vitendo, alisema chuo kiko katika hatua za kununua magari matatu aina ya KAMAZ sambamba na kuendelea kuboresha huduma ya intaneti kwa wanafunzi na watumishi.

Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, Mbunge wa Jimbo la Nungwi, Mdoe Haji Kombo aliishauri Serikali kuanzisha mfuko maalum utakaowawezesha vijana kupata elimu ya utalii na ukarimu ili kuongeza ushiriki wao katika sekta hiyo inayozidi kukua nchini.

“Sekta ya utalii inakua kwa kasi na inachochea maendeleo ya vijana. Serikali ianzishe mfuko kwa vijana wanaopenda kujiunga na sekta ya utalii ili waweze kupata unafuu wa elimu katika masuala ya utalii na ukarimu,” alisema Mbunge huyo.