* Control Numbe ni 986930000001 itasomeka BMH ORGAN TRANSPLANT. Mimi nimechangia Sh 100,000 imekubali. Nawe changia unachokiweza.

Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kuna nyakati taifa hulazimika kusimama na kujiuliza; je, tunathamini vya kutosha taasisi zinazookoa maisha ya wananchi wake? Leo, swali hilo linafaa kuulizwa kuhusu Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma, taasisi ambayo kwa miaka michache imeonyesha kuwa Tanzania inaweza kufanya yale yaliyokuwa yakionekana kuwa ndoto.

Sitanii, kwa muda mrefu, Watanzania waliamini kuwa huduma za kibingwa kama kupandikiza figo au kuweka uloto kwa watoto ni mambo ya India, Ulaya au Afrika Kusini. Mzazi alipokuwa akiambiwa mtoto wake anahitaji matibabu hayo, mara nyingi moyo ulipasuka kabla hata safari haijaanza. Ile kuambiwa tu kuwa mtoto ana ugonjwa wa Selimundu, nyumba ziliuzwa, mashamba yaliwekwa rehani na ndugu walitawanyika kutafuta fedha za matibabu kwa kumpeleka mgonjwa nje ya nchi.

Lakini leo mambo yanabadilika mbele ya macho yetu. Madaktari wa Tanzania, ndani ya Hospitali ya Benjamin Mkapa, wamefanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa 56. Huduma hii imeanza mwaka 2018. Hiyo si takwimu ndogo. Hayo ni maisha ya Watanzania 56 ambayo kama si kurejeshewa matumaini, yalikuwa mbioni kupotea. Hawa wamepandikizwa figo na kurudi kuwaona wazazi wao, ndugu, jamaa na marafiki. Ni wazazi waliorudi kuwalea watoto wao, ni Watanzania waliorudishwa katika uzalishaji wa taifa lao.

Sitanii, bado kuna jambo kubwa zaidi. Watoto 30 tayari wamewekewa uloto hapa hapa nchini. Haya ni mapinduzi ya kitabibu ambayo miaka michache iliyopita yangeonekana hadithi ya kufikirika. Leo yanafanyika Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa. Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, anasema kwa sasa baada ya utaalamu huu, hata Wizara ya Afya inaendelea na maandalizi ya kubadili Sera ya Afya ya Mwaka 2007.

“Sera hii ilijielekeza katika kutibu malaria, magonjwa ya kuharisha na mengine ya kawaida. Haikupata kufikiri kuwa Tanzania tunaweza kutoa huduma za kibingwa. Matibabu yaliyokuwa yanafanyika nje ya nchi, kwa sasa yanafanywa na madaktari Watanzania hapa kwetu Dodoma, Tanzania… kwa sasa tunalenga kujenga Jiji la Matibabu kwa ajili ya utalii wa tiba. Tunashirikiana na UDOM na hili litawezekana,” amesema Prof. Makubi alipokutana na Wahariri mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Katika hatua ya kuonyesha uongozi wenye kugusa maisha ya wananchi, Rais Samia Suluhu Hassan ametenga Sh bilioni 1.0 kusaidia matibabu ya watoto wanaopata tiba ya ugonjwa wa selimundu. Gharama ya kumtibu mtoto mmoja inafikia hadi Sh milioni 45, si kila mzazi anaweza kuzimudu gharama hizi. Huu si msaada wa kawaida alioutua Rais Samia kwa watoto wa Kitanzania. Ni ujumbe kuwa serikali imeamua kusimama upande wa uhai wa wananchi wake.

Lakini ukweli mmoja lazima usemwe wazi; vita hii bado haijaisha. Mahitaji yaliyopo yanaonyesha kuwa zaidi ya Sh bilioni 7 zinahitajika ili kuongeza idadi ya wagonjwa wanaoweza kupata huduma hizi muhimu. Hapa ndipo Watanzania tunapaswa kujiuliza; tutabaki watazamaji au tutakuwa sehemu ya historia hii?

Kila mfanyabiashara, kila kampuni, kila taasisi ya dini, kila benki na kila Mtanzania mwenye uwezo ana wajibu wa kushiriki. Si lazima mtu atoe mabilioni. Wengine watatoa milioni, wengine laki, wengine elfu kadhaa. Unaweza kuchangia hata Sh 1,000, wakichangia watu milioni 1.0 kila mmoja kiasi hicho, tayari itakuwa Sh bilioni moja. Lakini mchango wa kila mmoja unaweza kuokoa maisha ya mtoto ambaye leo amelazwa akisubiri tumaini.

Sitanii, tunapochangia huduma hizi, hatuchangii saruji wala majengo. Tunachangia uhai. Tunachangia mama asimzike mtoto wake. Tunachangia baba asiishi na majonzi ya kushindwa kumudu matibabu ya mwanawe.

Taifa kubwa halijengwi kwa maneno makali ya kisiasa pekee. Linajengwa kwa uwezo wa wananchi wake kusimama pamoja wakati wenzao wanapohitaji msaada. Leo, Hospitali ya Benjamin Mkapa imeonyesha uwezo. Serikali imeonyesha nia. Kilichobaki ni Watanzania kuonyesha moyo.

Tusisubiri mpaka ugonjwa huu ugonge mlango wa nyumba zetu ndipo tuone umuhimu wa huduma hizi. Leo ni mtoto wa mwenzako, kesho inaweza kuwa damu yako mwenyewe.

Sitanii. Tanzania inaandika historia mpya ya tiba barani Afrika. Tuamue kuwa sehemu ya historia hiyo, si watazamaji wake. Hospitali hii ya Benjamin Mkapa ilianzishwa Oktoba 13, mwaka 2015. Sasa inaadhimisha miaka 10 ya kutoa huduma. Hadi sasa Serikali imewekeza Sh bilioni 283. Kiasi hiki si haba. Ni uwekezaji mkubwa.

Prof. Makubi anaposema anataka kufanya utalii wa kimatibabu, hafanyi utani. Hadi sasa Hospitali ya Benjamin Mkapa imekwishahudumia wagonjwa 526 kutoka Comoro, wagonjwa 2,897 kutoka Burundi, mwaka jana imehudumia wagonjwa 18,000 kutoka nchi mbalimbali. Idadi ya Watanzania waliotibiwa, usipime.

Kwa msaada wa Japan imejenga kituo cha kupasua figo kilichogharimu Sh bilioni 28. Na sasa inajenga kituo cha uchunguzi wa saratani kwa Afrika Mashariki kwa gharama ya Sh bilioni 32.

Profesa Masumbuko Mwashambwa, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya figo anayefanya upasuaji pale Hospitali ya Benjamin Mkapa, anasema kwa sasa watu zaidi ya milioni 850 duniani kati ya watu bilioni 8 wanaoishi katika dunia hii, wana matatizo ya figo. Magonjwa ya figo ni janga la kidunia.

Sitanii, mtaalamu wa kupandikiza uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, Dk. Stella Malangahe, akikusimulia ukubwa wa tatizo linalotokana na ugonjwa wa selimundu, unaogopa. Huu ni ugonjwa ambao mtoto anaishiwa damu, anadumaa katika ukuaji na unadhoofisha afya ya akili mara 10 zaidi ya mtoto asiye na ugonjwa huu, ila kupitia upandikizaji wa Uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, mtoto anapona.

Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi tano zinazoongoza duniani kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu (Sickle Cell), mara nyingi ikishika nafasi ya 4 au ya 5. Takwimu zinaonyesha nchi yetu ina zaidi ya wagonjwa 200,000, huku asilimia 15 ya Watanzania wakiwa na vinasaba vya ugonjwa huu. Ni hatari.

Kwa hakika magonjwa ya selimundu na figo ni janga la kitaifa. Gharama za matibabu ni za kutisha. Mgonjwa akipandikizwa Uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, gharama yake inakuwa kati ya Sh milioni 40 hadi Sh milioni 45. Angekwenda nje ya nchi, ingekuwa kati ya Sh milionii 60 hadi Sh milioni 80.

Mgonjwa anayebadilisha figo, pale Benjamin Mkapa inagharimu wastani wa Sh milioni 75, ilihali angekwenda nje ya nchi ingemgharimu Sh milioni 130. Kwa hakika hizi gharama si familia nyingi zinazoweza kuzimudu. Ndiyo maana katika kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya Hospitali ya Benjamin Mkapa kitakachofanyika Julai 15, 2026 jijini Dodoma, wanaomba msaada wa Watanzania kuchangia sehemu ya gharama.

Mbali na Serikali kuwekeza Sh bilioni 283 katika hospitali hiyo, kwa sasa wanatafuta Sh bilioni 7 tu, waweze kuongeza idadi ya vyumba vya kupasulia wagonjwa angalau kutoka viwili vya sasa hadi vitano, hali itakayoongeza idadi ya wagonjwa wanaopata huduma hii.

Katika kufanikisha hilo, wametengeneza namba ya malipo (control number) ambayo unaweza kuchangia hata Sh 500, utakuwa umeshiriki kuokoa maisha ya angalau Mtanzania mmoja. Control Number hiyo ni 986930000001 itasomeka BMH ORGAN TRANSPLANT.

Mimi nimechangia Sh 100,000 imekubali. Nawe changia unachokiweza, kisha unijulishe kupitia namba yangu iliyopo hapo juu, niueleze umma wema wako. Ukichanga zinakwenda moja kwa moja hospitali ya Benjamin Mkapa, haziji kwangu. Tuwaunge mkono Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, wapate hiyo Sh bilioni 7. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827