Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kuna msemo wa Kiswahili unaosema, “Ukiona simba anakuangalia, usianze kupambana naye kwa hasira; kwanza jiulize kwa nini amesimama mbele yako.”
Leo Tanzania imejikuta katika hali ambayo Seneti ya Marekani imewasilisha muswada unaopendekeza mapitio makubwa ya uhusiano kati ya Washington na Dodoma.
Muswada huu unataja uwezekano wa kuweka vikwazo kwa baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu, haki za kisiasa na kuzorota kwa demokrasia nchini Tanzania.
Muswada huo umeletwa na maseneta wawili kutoka vyama vinavyopingana nchini Marekani, Seneta Jeanne Shaheen wa Democratic na Seneta Ted Cruz wa Republican. Hii si hoja ya chama kimoja, bali ni ishara kuwa ndani ya mfumo wa kisiasa wa Marekani kuna makubaliano mapana kuhusu namna wanavyoitazama Tanzania kwa sasa.

Sitanii, naomba kwa unyenyekevu mkubwa na kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, kwa maslahi mapana ya taifa letu, kukishauri Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali. Najiuliza sasa, CCM inapaswa kufanya nini?
Jambo la kwanza ni kuepuka mtego wa jazba. Historia inaonyesha kuwa mataifa mengi yaliyoingia katika mvutano wa moja kwa moja na Marekani kwa misingi ya maneno makali, yalijikuta yakipoteza zaidi kuliko yalivyopata.
Marekani ni mshirika mkubwa wa Tanzania katika afya, biashara, uwekezaji, elimu na usalama. Kwa miongo mingi, Watanzania wamefaidika na programu mbalimbali za ushirikiano zilizogusa maisha ya mamilioni ya wananchi.
Jambo la pili ni kutenganisha maslahi ya taifa na maslahi ya wanasiasa binafsi. Hata wachambuzi wengi wa masuala ya diplomasia wanaeleza kuwa vikwazo vinavyojadiliwa vinaelekezwa zaidi kwa watu binafsi kuliko taifa lote.
Hivyo, si busara kuifanya Tanzania ionekane inapambana na Marekani kwa ajili ya kutetea watu wachache wanaotajwa katika mijadala hiyo. Zipo njia za kuwatetea, na jamii ikazielewa, ikiwamo kusahihisha yanayolalamikiwa.
Jambo la tatu ni kuipa nafasi diplomasia. Kwa bahati nzuri, Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo, tayari ameonyesha njia sahihi kwa kusisitiza mawasiliano ya kidiplomasia badala ya majibizano ya hadharani. Hiyo ndiyo lugha inayopaswa kutawala.
Sitanii, lakini pia CCM inapaswa kutambua kuwa dunia ya leo si ya kuficha mambo. Taarifa za uchaguzi, haki za binadamu na utawala bora husafiri kwa kasi kuliko wakati mwingine wowote katika historia.
Njia bora ya kujibu tuhuma si kutoa kauli kali, bali kuonyesha kwa vitendo kuwa taasisi za nchi zina uwezo wa kuchunguza malalamiko, kuwawajibisha wahusika na kurekebisha kasoro zilizojitokeza. Hakuna uchaguzi usiokuwa na kasoro popote duniani, ila ikitokea wahusika huwajibishwa na watu huridhika wakiona aliyeharibu anawajibishwa.
Kama kweli kuna hoja zinazohitaji ufafanuzi kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, basi Tanzania itanufaika zaidi kwa kuonyesha uwazi kuliko kujifungia. Tayari Tume ya Jaji Chande Othman imekuja na majibu mengi kati ya hoja zinazoendelea kuzunguka. Mimi kama mtaalamu wa mawasiliano ya umma, naamini aliyeshauri taarifa hii isiwafikie wananchi, anatengeneza matatizo makubwa kuliko suluhisho.
Sitanii, inawezekana aliyeshauri amebobea katika eneo lake la kazi, lakini basi atuombe ushauri sisi ambao tupo kwenye taaluma hii kwa zaidi ya miaka 32 sasa. Tunafuatilia historia ya mambo yanavyokwenda duniani.
Katika hali ya sasa, viongozi wetu wanaweza kupigiwa simu kwa WhatsApp na wahusika wakawaambia ‘wasitubabaishe’, lakini uhalisia huu si wakati wa kutumia mabavu. Tunafahamu kuwa nyuma ya muswada huu kuna karata ya vita ya kiuchumi.
Ipo miradi inayowatoa macho Wamarekani, kama vile mradi wa Uranium wa Mkuju, Ruvuma; gesi ya LNG ya Lindi; mradi wa Nickel wa Kabanga-Ngara na hofu juu ya uwekezaji mkubwa unaoletwa na China nchini Tanzania. Hii iko wazi, ila ukila na kipofu, dokoa. Hakikisha humshiki mkono; atashituka kuwa unabugia minofu, yeye unamsogezea mifupa kwa kuwa haoni.
Sitanii, Mwalimu Julius Nyerere aliliona hilo. Ndiyo maana akatangaza sera rasmi ya Tanzania kuwa ni “Kutofungamana na Upande Wowote.” Hii tuendelee kuiimba. Wakija Wamarekani tuwafungulie milango, tuwape ushirikiano hadi washangae. Wakija Warusi au Wachina, tuwafungulie milango na tuwape ushirikiano hadi washangae. Mwishowe watatuelewa.
CCM imeiongoza Tanzania kwa zaidi ya nusu karne. Uzoefu huo mkubwa wa uongozi unapaswa kuonekana katika busara, si katika hasira. Katika mgogoro huu, ushindi si kuishinda Marekani kwa maneno. Ushindi ni kuilinda Tanzania dhidi ya madhara ya kidiplomasia, kiuchumi na kisiasa yanayoweza kuepukika. Tukumbuke walikopitia Venezuela, wanakopitia Cuba au Iran. Sisi hatuna msuli kama hao, ila wamewatesa!
Sitanii, rungu la Marekani si jambo la kubeza. Njia sahihi si kupambana nalo. Njia sahihi ni kutumia diplomasia, uwazi na maridhiano ili kulifanya lisipigwe kabisa. Taifa likibaki salama, kila Mtanzania anashinda.
Sitanii, binafsi nina imani kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Nazielewa 4R zake. Naielewa kauli yake ya maridhiano. Lakini nafahamu pia wahafidhina wapo ndani ya CCM. Wanatoa ushauri wa kujipiga kifua bila kuangalia nyuma au pembeni. Rais Samia umetutoa mbali, na hili unayo nafasi ya kulimaliza.
Chondechonde tusitumie mabavu. Wahenga walitwambia, funika kombe mwanaharamu apite. Upepo wa kisulisuli si wa kudumu. Hata hizo zinazoitwa kesi za kisiasa zinaweza kumalizwa kiungwana kama utamaduni wetu sisi Watanzania ulivyo.
Naamini iwe CCM, CHADEMA, ACT-Wazalendo au hao wengine, kuzungumza kwa nchi yetu si mwiko. Tuzungumze, tuwaite wageni kwenye sherehe ya maridhiano. Mzee Amani Abeid Karume na Maalim Seif waliweza. Mzee Benjamin Mkapa na Profesa Ibrahim Lipumba walizungumza. Hakutakuwa na ajabu Rais Samia na Lissu kuzungumza.
Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827

